Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 2:31 pm

NEWS: MAZUNGUMZO KUHUSU MGOGORO WA BURUNZI KUFANYIKA KWA SIKU 13 ARUSHA.

ARUSHA: MAZUNGUMZO kuhusu mgogoro wa kisiasa Burundi, yanatarajiwa kufanyika kwa siku 13 kuanzia wiki hii jijini Arusha, chini ya Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu Tanzania, Benjamin Mkapa.

Hayo yamethibitishwa na Mkapa, ambaye ni mpatanishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) aliyekabidhiwa jukumu la Burundi. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mawasiliano kwenye Sekretarieti ya EAC, Richard Owora Othieno, mazungumzo hayo yanatarajiwa kuwa na maamuzi muhimu.

Hata hivyo, bado haijaelezwa wazi ajenda hasa za mazungumzo yajayo na hata pande zitakazoshirikishwa katika mazungumzo hayo. Serikali ya Burundi ilikataa kushiriki katika mazungumzo ya moja kwa moja na upinzani, ikiutuhumu kwamba ulihusika katika jaribio la mapinduzi yaliyofeli ya Mei mwaka 2015.

Burundi iliingia katika machafuko Aprili mwaka 2015 baada ya chama tawala cha CNDD-FDD, kumuidhinisha Pierre Nkurunziza kuwania tena urais katika uchaguzi mkuu uliopita, ikiwa ni kwa mara ya tatu mfululizo.

Wapinzani wa kisiasa waliitaja hatua ya Rais Nkurunziza kushiriki katika uchaguzi huo kwamba ilikiuka Katiba na hati ya Makubaliano ya Amani ya Arusha, lakini Serikali ya Burundi ilisisitiza kwamba haijakiuka sheria.