Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 9:30 pm

NEWS: MAVUNDE AWATAKA VIJANA KUCHANGAMKIA FURSA ZA BOMBA LA MAFUTA.

TANGA: Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu(Kazi,Vijana na Ajira) Mh. Anthony Mavunde leo amezindua programu ya Urasimishaji Ujuzi kwa Vijana ambao wana ujuzi lakini hawakupitia katika mfumo rasmi wa mafunzo ya Ufundi(Recognition of Prior Learning).

Ufunguzi huo wa Program hii ya Urasimishaji Ujuzi ambao unagharamikiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu umefanyika leo katika Chuo cha VETA Jijijni Tanga na kujumisha jumla ya Vijana 701 kutoka mikoa ya Tanga,Kilimanjaro,Arusha na Manyara wanatarajiwa kunufaika na mpango huo.

Akizungumza na Vijana hao, Mh.Mavunde amesema serikali inatekeleza mpango mkubwa wa ukuzaji ujuzi kwa Vijana unaolenga kuwafikia takribani Vijana Milioni 4 nchi nzima kwa lengo la kuwajengea ujuzi stahiki utakaowasaidia kupata Ajira na kujiajiri wenyewe.

Aidha Naibu Waziri Mavunde amewataka Vijana wote kuchangamkia fursa mbalimbali zitokanazo na ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima,Uganda-Tanga ambapo serikali kuu na serikali ya Mkoa wameendelea kujenga mazingira rafiki ya kuhakikisha Vijana wanafikia malengo yao.

Wakizungumza baada ya kuzinduliwa program hiyo, Vijana hao wameishukuru Serikali kwa Mpango huu wa urasimishaji ujuzi ambao unawapa fursa ya kupewa cheti cha Ufundi kutoka VETA bila kupitia utaratibu wa kawaida wa masomo ambapo takribani Vijana 3900 watanufaika na Mpango huu nchi nzima.