Home | Terms & Conditions | Help

November 29, 2024, 12:34 am

NEWS: MATAIFA 128 YAPINGA UWAMUZI WA MAREKANI JUU YA JERUSALEM

New York: Nchi wanachama za umoja wa Mataifa zimekaidi vitisho vya Serikali ya Marekani na kupiga kura ya ndio kuidhinisha azimio linalotupilia mbali tangazo la rais Donald Trump kuutambua mji wa Jerusalem kama makao makuu ya Israel.

Nchi wanachama 128 zilipiga kura ya ndio dhidi ya kura 9 zilizopinga huku nchi 35 zikijiondoa kushiriki kwenye kura hiyo.

Hata hivyo mamlaka ya Palestina imesema licha ya azimio hilo kuungwa mkono, halina nguvu yoyote dhidi ya hatua ya Marekani kuutambua mji wa Jerusalem kama makao makuu ya Israel'.

Tayari nchi kadhaa zimetangaza kupunguza hadhi ya balozi zake nchini Israel kama kuonesha mshikamano na watu wa Palestina.

Azimio hilo limepitishwa licha ya vitisho vya rais Donald Trump ambaye juma hili alitishia kusitisha misaada yake ya kifedha kwa nchi wanachama ambazo zingepiga kura kuunga mkono azimio hilo.

Akizungumza kwenye baraza hilo kabla ya kura yenyewe, balozi wa Marekani kwenye umoja wa Mataifa Nikki Haley aliyaonya mataifa hayo na kusisitiza kuwa Serikali yake haitasahau kitendo cha kidhalimu kilichofanywa na nchi wanachama.

Mpatanishi mkuu wa Serikali ya Palestina Saeb Erakat amelaani uamuzi wa Serikali ya Marekani lakini hata hivyo akapongeza kura hiyo akisema imeonesha umoja wa Mataifa unaheshimu sheria.

Erakat amesema “ni aibu kwa nchi ambazo ziliamua kuunga mkono uamuzi wa Marekani unaifanya Israel kukalia maeneo ya watu kwa nguvu”.