Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 3:34 am

NEWS : MAKAMU WA RAIS ALIYETIMULIWA NA RAIS MUGABE AKIMBIA NCHI

Makamu wa Rais wa Zimbabwe aliyeuzuliwa akimbia nchi

Makamu wa Rais wa Zimbabwe aliyefutwa kazi na kutimuliwa ndani ya chama tawala Zanu-PF hivi karibuni amekimbilia uhamishoni akidai kuwa maisha yake yamo hatarini.

Haijabainika ni jinsi gani Emmerson Mnangagwa amefanikiwa kuondoka nchini Zimbabwe kinyemela, lakini baadhi ya vyanzo vya habari vinasema ameondoka nchini kupitia nchi jirani ya Botswana.

Jumatatu iliyopita, Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe alimpiga kalamu nyekundu makamu wake Emmerson Mnangagwa, kutokana na kile kilichotajwa kama ukosefu wa uaminifu na heshima kwa rais na kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Siku iliyofuata, yaani Jumanne, Mnangagwa alizuiwa na vyombo vya usalama kuondoka nchini kuelekea Msumbiji lakini jana Jumatano akafanikiwa kukimbilia uhamishoni.

Rais Mugabe na mkewe Grace

Mnangagwa mwenye umri wa miaka 75 amekuwa akionekana kama mmoja wa wanasiasa waliotarajiwa kumrithi Rais Mugabe, na kufutwa kwake kazi kunaonekana ni njia ya kumuondolea kizuizi mke wa rais Robert Mugabe, Grace Mugabe, aweze kurithi mikoba ya mumewe.

Hata hivyo Makamu wa Rais wa Zimbabwe aliyepigwa kalamu nyekundu ameapa kwamba anapanga mikakati na karibuni hivi atarejea nchini kuangusha utawala wa Rais Mugabe.