Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 6:44 pm

NEWS: MAJALIWA AWAPA ONYO WATUMIAJI VIBAYA WA MITANDAO

Dar es Salaam: Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewapa onyo watumiaji vibaya wa mitandao ya kijamii huku akisema Serikali itaendelea kuwachukulia hatua za kisheria wanaotumia mitandao ya kijamii kwa lengo la kuvuruga amani ya nchini

“Nitoe onyo kwa wale wote watakaoendelea kutumia mitandao hii vibaya watambue kwamba sheria zipo na zitaendelea kusimamiwa na kila sekta,” amesema.

Amewataka wananchi kutumia fursa za Teknolojia ya Mawasiliano (Tehama) kuongeza uzalishaji kwenye shughuli za kiuchumi na kujiongezea kipato kwa njia za halali.

Ametoa kauli hiyo leo wakati akitoa tuzo kwa washindi wa shindano la Tehama kwa wanafunzi wa vyuo vikuu mwaka 2018/19 lililoendeshwa na kampuni ya simu ya Huawei.

Amesema mitandao pamoja na teknolojia ya mawasiliano ina mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya Taifa endapo itatumika katika shughuli za uzalishaji na si vinginevyo.

Amesema kutokana na Tehama kuwa ngeni nchini, kuna fursa nyingi ambazo baadhi ya watu wamekuwa wakizitumia vibaya kwa lengo la kuhamasisha vitendo vya uvunjifu wa amani.

Majaliwa amesema matumizi ya Tehama katika shughuli za Serikali yamechangia kuongeza ufanisi wa ukusanyaji mapato pamoja na kupunguza gharama za utendaji.