- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: MAGUFULI,MUSEVENI WAWABANA MAWAZIRI
RAIS John Magufuli na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni wamewaagiza mawaziri wa nchi hizo mbili kujadiliana juu ya namna ya kuongeza biashara kati ya nchi hizo ili kupata manufaa makubwa zaidi ya uhusiano na ushirikiano wa kidugu uliopo.
Viongozi hao walitoa kauli hiyojana baada ya kufanya mazungumzo rasmi na kisha kuzungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ndogo ya Masaka nchini Uganda ambako Rais Magufuli ameendelea na ziara yake rasmi ya kiserikali ya siku tatu.
Akisisitiza juu ya agizo hilo, Rais Magufuli alisema kwa muda mrefu biashara kati ya Tanzania na Uganda imekuwa ni takribani Sh bilioni 200 kwa mwaka kiasi ambacho ni kidogo mno ikilinganishwa na fursa zilizopo, uhusiano na ushirikiano wa kidugu uliojengwa tangu enzi za Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
“Tumewaagiza mawaziri na wataalamu wakae na waangalie vikwazo vyote vinavyosababisha tufanye biashara kwa kiasi kidogo, wakishajadili watatuambia tufanye nini. “Tunataka kuona biashara ya Tanzania na Uganda inakua, hivi sasa Uganda imewekeza Dola za Marekani milioni 47 tu nchini Tanzania na kuzalisha ajira 146,000, kiasi hiki ni kidogo sana, ni lazima tuongeze,” amesema Rais Magufuli.
Kuhusu hatua ambazo Tanzania imeanza kuchukua Rais Magufuli alisema ni pamoja kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma umbali wa kilometa 726. “Serikali imekarabati reli iliyopo, pamoja na kivuko cha mabehewa ya treni cha Umoja katika Ziwa Victoria ili kuwezesha mizigo ya kutoka bandari ya Dar es Salaam kufika Kampala kwa gharama nafuu na pia inaendelea kujenga na kuimarisha barabara za mpakani.
“Napenda pia kukushukuru Rais Museveni kwamba Serikali yako sasa itajenga kipande cha kilometa 11 za reli kutoka Portbell hadi Kampala, na sisi tumeamua kuweka bandari kavu pale Mwanza ili wafanyabiashara wa Uganda wasisumbuke kwenda hadi Dar es Salaam, mizigo yao wataipata Mwanza, hii ni njia ya uhakika na nafuu ya kusafirisha mizigo,” ameongeza Rais Magufuli.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Rais Magufuli alieleza kuwa Tanzania imejipanga kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Uganda kwa kuhakikisha miradi mbalimbali inakwenda vizuri, ikiwemo kituo cha pamoja cha huduma za mpakani na mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania.
Kwa upande wake Rais Museveni alimpongeza Rais Magufuli kwa juhudi kubwa anazozifanya kupambana na rushwa na kuimarisha uchumi, na amemuagiza Waziri wake wa Ujenzi na Uchukuzi, Monica Ntege kuharakisha mchakato wa ujenzi wa kipande cha reli cha kilometa 11 kutoka bandari ya Portbell hadi Kampala ili usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli kutoka Bandari ya Dar es Salaam uanze mara moja.
Rais Museveni alisisitiza kukuzwa kwa biashara kati ya Tanzania na Uganda hasa wakati huu ambapo Uganda inahitaji kununua gesi ya Tanzania kwa ajili ya viwanda vyake vya mbolea na chuma na pia kurudisha historia ambapo Uganda ilikuwa mnunuzi mkubwa wa bidhaa za Tanzania.
Kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari, marais wote wawili walishuhudua utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Shirika la Utangazaji wa Uganda (UBC) na makubaliano kati ya Jeshi la Polisi la Tanzania na Jeshi la Polisi la Uganda.