Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 7:54 pm

NEWS: MAGUFULI AMUAGIZA LOWASSA KUWATULIZA WAPINZANI

Dar es Salaam: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John pombe Magufuli amemtaka waziri mkuu wa zamani, Edward Lowasa kuwaambia wanachama wengine wa upinzani anaowaongoza watulie “la sivyo wataishia gerezani”.

Rais ametoa kauli hiyo leo Novemba 27 baada ya kumsifu Lowassa, aliyekuwa waziri mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne, kuwa ni mwanasiasa mstaarabu ambaye alionyesha utulivu hata baada ya kushindwa katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015 mpaka kipindi hichi.

"Ninakupongeza sana (Lowassa). Hii ndiyo Tanzania mpya tunayoitaka. Vyama vyetu visiwe chanzo cha kututenganisha bali viwe chachu ya kuleta maendeleo," amesema Magufuli.

"Nimezungumza hili kwa heshima kubwa ili ukawashauri wale unaowaongoza watulie vinginevyo wataishia kwenye magereza."

Alisema hayo katika uzinduzi wa maktaba ya kisasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) leo Jumanne (Novemba 27) uliohudhuriwa na Lowassa, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.

Viongozi kadhaa wa upinzani, hadi sasa hasa Chadema wana kesi za aina tofauti katika mahakama mbalimbali nchini; baadhi wakishtakiwa kwa uchochezi, wengine kwa kutoa maneno yasiyofaa dhidi ya Rais na wengine kwa kufanya mikusanyiko bila ya kibali.

Hata na Wiki iliyopita, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alifutiwa dhamana pamoja na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko kutokana na kukiuka masharti ya dhamana katika kesi inayowakabili ya kufanya mikusanyiko kinyume cha sheria.

Akizindua maktaba hiyo ya kisasa yenye uwezo wakuchukua wanafunzi 2,100 na kutunza vitabu 800,000, Rais Magufuli amesema heshima iliyojengwa na UDSM inatakiwa iendelee kuwepo na wanafunzi wapate yanayostahili kwa wakati.

Amesema maktaba hiyo ni nyumba ya maarifa na ni kitu muhimu kwa maendeleo ya kielimu kwa sababu inatoa utulivu wa mtu kujisomea na kupata maarifa.

Rais Magufuli amesema kuanzia mwakani Watanzania watakuwa wakinufaika na mafunzo ya uhudumu wa maktaba kupitia ufadhili uliotolewa na serikali ya China

"Jukumu letu kama nchi ni kuitumia misaada hii vizuri ili iweze kuleta faida kwa manufaa ya Watanzania. Maktaba hii inatakiwa iwe ukumbusho wa W atanzania na watu wengine kutoka nchi jirani wanaokuja kututembelea," amesema.

"Nitasikitika sana kama siku moja nikija nikakuta maktaba hii imechorwachorwa na makaratasi yaliyopo katika shelf (kabatini) yamechanwachanwa. Badala yake tuitunze na iwe kumbukumbu ya ushirikiano wetu na serikali ya watu wa China."

Mbali na hilo pia Magufuli amesema kama nchi itaendelea kushirikiana na nchi mbalimbali katika kuleta maendeleo baina ya nchi hizo.

Kuhusu mikopo ya wanafunzi, Rais alisifu Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kwa kuitoa kwa wakati na kutaka iendelee.

"Nimeambiwa suala la mikopo ni asilimia 60 tu ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza ndiyo wamepata, endeleeni kushughulikia ili wapate mikopo itakayowasaidia kupata elimu," amesema Mgufuli.