Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 9:30 am

NEWS: MADIWANI ILALA WATWANGANA NGUMI HADHARANI

Dar es Salaam: Leo katika uchaguzi wa Naibu Meya wa Manispaa ya ilala Vurugu zilitawala na kusababisha watu kutwangana ngumi hadharani, vurugu hizo zilimuhusisha Diwani wa Tabata (Chadema) Patrick Assenga aliyechapana makonde na baadhi ya madiwani wa CCM katika Ukumbi wa Anatouglo Jijini Dar es salaam.

Akizungumza na waandishi wa Habari, Assenga amesema chanzo cha vurugu hizo ni baadhi ya kura kuharibika lakini mkurugenzi wa manispaa hiyo, Jumanne Shauri amepinga na kusema hakuna kura iliyoharibika.

“Mzozo ulianzia katika chumba cha majumuisho ya kura, nikiwa kama mwangalizi wa kura niliona baadhi ya kura zimeharibika na hazifai kwa mujibu wa uchaguzi, lakini Shauri na watu wengine walikataa,” amesema Assenga.

“Niliamua kuzishikilia zile kura nne zilizoharibika baada kuona hivyo Shauri alitoka nje ya chumba na kuwaita polisi ambao walikuja kuninyang’anya zile kura na kunitoa nje ya chumba.”

Amesema baada ya kutolewa katika chumba hicho alikwenda kuzungumza na madiwani wenzake wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ndipo wajumbe wa CCM walipomfuata na kuanza kurushiana maneno, kisha kuanza kuchapana makonde.

“Hii ya leo kali, bado tuna safari ndefu katika chaguzi hapa nchini. Tuliona dalili mapema za kuvuruga uchaguzi huu kwa polisi kuwa wengi kupita kiasi,” amesema Assenga.

Katika uchaguzi huo Diwani wa Vingunguti (CCM), Omar Kumbilamoto ameibuka mshindi katika uchaguzi wa naibu meya wa manispaa ya Ilala.

Uchaguzi huo ulifanyika baada ya Kumbilamoto aliyekuwa naibu meya Ilala kwa tiketi ya CUF kujiuzulu na kuhamia CCM, akieleza ameshindwa kuwatumikia wananchi kutokana na chama chake kuwa na mgogoro wa uongozi.

Akizungumzia uchaguzi huo, Shauri amesema ulikuwa wa haki na ulifuata taratibu zote na wajumbe walikuwa 52. CCM 26 na Ukawa kwa maana ya CUF na Chadema 26.

Amesema baada ya mchakato wa kuhesabu kura kukamilika, Kumbilamoto alipata kura 27 wakati Rajab Penza wa CUF akipata 25.

Hata hivyo, Shauri amekiri vurugu kutokea akidai zimesababishwa na Assenga lakini polisi walifanikiwa kumdhibiti.

“Alichokuwa akidai Assenga ni kwa nini baadhi ya wajumbe wamepiga pembezoni mwa nembo. Utaratibu uliokuwapo ni kuwa watu kuandika jina la mgombea iwe nyuma au mbele kwa sababu karatasi ilikuwa ‘plain’,” amesema.

“Nawaambia madiwani wa Ilala, uchaguzi umekwisha kilichobaki ni kufanya kazi na kuwa kitu kimoja.”