Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 7:48 pm

NEWS: MABORESHO YA MWONGOZO WA UTOAJI HUDUMA ZA KIELIMU KUSAIDIA WENYE UONI HAFIFU.

Maboresho ya mwongozo wa utoaji huduma za kielimu kusaidia kutatua changamoto za mazingira ya kielimu kwa wenye ulemavu wa ngozi (ualbino) na uoni hafifu.

Akizungumza Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Wenye Ulemavu Bi. Magreth Malunda alisema kuwa Serikali imekuwa ikisirikiana kwa karibu na Shirika la Kimataifa la Kutetea haki za wenye ualbino Duniani (Under the Same Sun) pamoja na wadau mbalimbali katika harakati za kutatua changamoto za kielimu zinazowakabili wanafunzi wenye ualbino, hususan suala la uoni hafifu.

“Mwongozo huo utakuwa ni nyenzo muhimu katika utoaji huduma za kielimu kwa watoto wenye ualbino na uoni hafifu hapa nchini, maana utasaidia kutambua mahitaji yao muhimu,” alisema Malunda.

Kwa upande wake Mwanasheria wa Shirika la Under the Same Sun, Bw. Madulu William alisema kuwa matatizo wanayokumbana nayo wanafunzi wenye ualbino ni pamoja na kushindwa kusoma vizuri mitihani na mwandiko ubaoni wanapokuwa madarasani, hivyo kusababisha wengi wao kushindwa kufanya vizuri katika masomo.

“Jambo la msingi ni kuhakikisha mwongozo unakuwa na njia bora ya kuwawezesha walimu kujua jinsi watakavyoweza kuwajumuisha wanafunzi wenye ualbino na uoni hafifu wanapata fursa sawa kama walivyo wanafunzi wengine,” alisema William.

Naye Meneja Mradi Jumuishi wa Watu wenye Ualbino (KCBRP) Bw. Florence Rugemalira alisema kuwa ni vyema jamii ikaelimishwa juu ya watu wenye ulemavu ualbino na uoni hafifu ili waweze kutambua kuwa wanaouwezo kama wengine katika kupata elimu.

Warsha hiyo imehusisha Wizara mbalimbali na wadau wanaofanya kazi kwa ukaribu na watu wenye ualbino ambapo walikutana kwa siku mbili kupitia na kurekebisha mwongozo wa utoaji elimu kwa wanafunzi wenye ualbino na uoni hafifu.