Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 5:32 am

NEWS : MAAFISA WA NGAZI ZA JUU SAUDIA NA ISRAEL WAKUTANA MAREKANI

Maafisa wa ngazi za juu wa Saudi Arabia na Israel wakutana Marekani

Maafisa wa ngazi za juu wa Saudi Arabia na Israel wakutana Marekani

Tzipi Livni Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni wa Israel amekutana na Turki al Faisal, mkuu wa zamani wa shirika la kijasusi la Saudi Arabia.

Livni ameashiria mkutano huo katika ujumbe aliotuma katika akaunti yake ya Twitter na kusema kuna uwezekano wa kuwepo uhusiano wa kawaida baina ya Israel na nchi za Kiarabu. Hii ni katika hali ambayo utawala bandia wa Israel umekuwa ukitekeleza jinai katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu ambapo Wapalestina wamepokonywa ardhi zao na kufanywa wakimbizi.

Katika miezi ya hivi karibuni kumeshuhudiwa ongezeko la mikutano ya siri na ya wazi baina ya viongozi na maafisa wa ngazi za juu wa utawala wa Kizayuni wa Israel na Saudi Arabia katika fremu ya kuandaa uhusiano wa kawaida baina ya pande mbili.

Nchi kadhaa za Kiarabu waitifaki wa Saudia hasa Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu ziko katika mkakati wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni na hivyo zinalenga kujiunga na Misri na Jordan ambazo zina uhusiano rasmi na utawala huo bandia.

Mkutano wa siku za nyuma baina ya Turki al Faisal na Tzipi Livni

Nchi hizo za Kiarabu zinaunga mkono uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unawakandamiza Wapalestina na kuwaangamiza kwa umati. Aidha utawala wa Kizayuni wa Israel unakalia kwa mabavu ardhi za Palestina hasa mji wa Quds uliopo Msikiti wa al Aqswa ambao ni Qibla cha kwanza cha Waislamu.

Tayari Saudi Arabia inashirikiana na Israel katika kueneza migogoro na kuibua makundi ya kigaidi ambayo yamevuruga amani Syria na Iraq. Aidha tawala za Riyadh na Tel Aviv zinashirikiana katika hujuma dhidi ya Yemen tokea Machi 2015 ambapo watu zaidi ya 13,000, wengi wakiwa ni watoto, wameuawa na mamilioni ya wengine kuachwa bila makao.