- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: LUGOLA AFUATILIA MAAGIZO YAKE YA DHAMANA KWA POLISI YA SAA 24
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewasili mjini Bukoba Mkoani Kagera leo, kwa ajili ya kuanza ziara yake ya kikazi ya siku nane kwa kutembelea Wilaya zote za Mkoa huo akisikiliza kero za wananchi pamoja na kufuatilia maagizo yake aliyoyatoa kwa vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo ndani ya Wizara yake. Waziri Lugola anatarajia kuanza ziara hiyo rasmi kesho Januari 2, 2019 mjini Bukoba kwa kukutana na Mkuu wa Mkoa pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na kupokea taarifa ya Kamati hiyo, kabla ya kuanza kuzungumza na Wakuu wa vyombo vyake na baadaye kuzungumza na Baraza la Askari na Watumishi wote wa Wizara hiyo waliopo mjini humo.
Pia Lugola alisema lengo la ziara hiyo ni kufuatilia maagizo yake mbalimbali ambayo aliyatoa mwaka jana 2018 katika mikutano yake kama yalifanyiwa kazi na viongozi wa Taasisi anazoziongoza au yalipuuzwa, yakiwemo ya dhamana zitolewe saa 24 katika vituo vyote vya polisi nchini, na pia kupiga marufuku tabia ya baadhi ya Polisi kubambikizia kesi wananchi, na pamoja na agizo la pikipiki zote zilizopo vituoni ziondolewe.
Akizungumza na Mwandishi wa habari hii, leo, Lugola amesema baada ya kuzungumza na Askari na Watumishi wa Wizara yake pamoja na kupokea changamoto zao, atafanya mkutano mkubwa wa hadhara wa wananchi utakaofanyika uwanja wa uhuru mjini humo ili aweze kusikiliza na kuzitatua kero mbalimbali zinazowakabili. “Nitafanya mkutano mkubwa wa hadhara utakaofanyika Uwanja wa Uhuru eneo la Mayunga hapa mjini Bukoba, ambapo utaanza saa 10:00 hadi 12:00 jioni, hivyo nawaomba wananchi wa mji huu wajitokeze kwa wingi kunisikiliza kile ambacho nimepanga kuwaambia na pia nitawapa nafasi wananchi waulize maswali bila woga, waniambie kero zao nami nitazitatua katika mkutano huo,” alisema Lugola.
Lugola alisema katika ziara yake aliyoifanya mwaka jana Mkoani Kigoma aligundua wananchi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali hivyo hawezi kulala akiwa ofisini, lazima afanye ziara nchi nzima kuwasaidia wananchi kutatua kero zao ambapo wengi wao wakiwalalamikia Polisi wakiwaonea.
Waziri Lugola ameongeza kuwa, kupitia mikutano yake ya wananchi mkoani Kigoma ndipo ameamua kufanya ziara ya pili kwa kuutembelea Mkoa wa Kagera ambao changamoto zake zinafanana kwa sehemu kubwa kwa kuwa mikoa hiyo ni ya mipakani na changamoto kubwa ni uwepo wa wahamiaji haramu pamoja na matukio kadhaa ya ujambazi ambayo kwa kiasi kikubwa Serikali inaendelea kuyadhibiti.
“Wananchi wanapojitokeza kwa wingi inasaidia kusikiliza matatizo yao yanayowakabili, ndio mana nimepanga kufanya ziara kama hizi nchi nzima, hii inasaidia sana kujua matatizo mbalimbali ya wananchi pamoja na kuangalia utendaji kazi wa Taasisi zangu zilizopo ndani ya Wizara hii, na hakika Serikali ya Dokta Magufuli inawajali wananchi wake ndio mana inawafuata mahali walipo, ili wazungumze na Serikali yao uso kwa uso,” Alisema Lugola.