Jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa itatoa hukumu juu ya hoja za awali za mapingamizi baada ya kutoa taarifa (NOTICE) kama ulivyo utaratibu wake. Na kwamba, kwa mujibu wa kanuni za Mahakama ya Rufaa hukumu inatarajiwa kutolewa ndani ya siku 14 kuanzia tarehe shauri liliposikilizwa.
Katika maombi yake ya msingi, bodi hiyo inaiomba mahakama ya rufaa kutengua uamuzi katika shauri Na. 80/2017 lililofunguliwa kwenye Mahakama Kuu Oktoba 2017, na Bodi ya Wadhamini inayomuunga mkono Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.
Mahakama Kuu mbele ya Jaji Wilfred Dyansobera ilitoa amri ya kumzuia Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kutoa fedha za ruzuku ya CUF kwa Pro. Lipumba na wenzake, hadi pale maamuzi ya shauri Na. 21/2017 dhidi yake na Mwanasheria Mkuu wa Serikari (CAG) kuhusu tuhuma za kutoa fedha za ruzuku Sh. 369 milioni, yatakapotolewa.
Kesi hiyo ilifunguliwa na Bodi ya Wadhamini ya CUF inayomuunga mkono Maalim Seif, ikidai kuwa fedha hizo hazijulikani matumizi yake, pamoja na kutokuwa kwenye mikono salama kutokana kwamba Prof. Lipumba ambaye bodi yake ilikabidhiwa fedha hizo, alivuliwa uanachama.
Mvutano wa bodi hizo mbili ulikuja baada ya uwepo wa mgogoro wa kiungozi uliokikumba chama hicho, ambapo upande wa Maalim Seif unadai kuwa Prof. Lipumba si mwenyekiti halali kufuatia kuvuliwa uanachama wa CUF, wakati Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ikimtambua kuwa kiongozi halali pamoja na bodi yake.