Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 6:54 pm

NEWS: LIJUALIKALI AFUNGUKA SABABU ZITAKAZOMFANYA AIHAME CHADEMA.

Mbunge wa Kilombero (Chadema), Peter Lijualikali, ameibuka na kutaja sababu inayoweza kumshawishi kujiunga na chama tawala hicho.


Akizungumza na waandishi wa habari, muda mfupi baada ya kukagua mradi wa reli ya kisasa (SGR), kipande cha Dar es Salaam-Kilosa, akiwa miongoni wa wabunge wa kundi la maendeleo endelevu bungeni walioutembelea, Lijualikali alisema anaweza kuihama Chadema na kujiunga na CCM ikiwa serikali itaendelea kutekeleza miradi mikubwa kama huo.


“Wanaosema nitahamia CCM ni jambo jema kuwa wanapenda nihamie CCM, ila nitahamia CCM kama tu nitaona kuna sababu za msingi na mengine ya msingi yanafanyika," alisema.


Lijualikali alisema kuwa kama serikali itaendelea kutekeleza miradi mingine mikubwa nchini, hatakuwa na sababu za kukataa kukihama chama chake.


Hata hivyo, mbunge huyo alisema anakwazwa na kitendo cha kutishwa na kukamatwa kamatwa kwa viongozi wa upinzani nchini.


"Nitahamia CCM kama nitaona sababu za msingi sana na mengine ya msingi, lakini si huku kutishana na kufungwa fungwa na kufia jela," alisema Lijualikali.


Alisema hayuko Chadema kwa bahati mbaya na anaamini kwa sasa ni sehemu sahihi kuwapo.


Akizungumzia mradi huio, Lijualikali alisema: "Mradi huu ni kitu endelevu, kitu ambacho tunaamini hata Chadema tukichukua nchi, hatutaing'oa reli, itabaki."

Alisema mafanikio ya mradi huo yataonekana mara utakapokamilika nchi nzima na mizigo kuanza kusafirishwa kwenda nchi mbalimbali.


“Baada ya mizigo kuanza kusafirishwa, nchi itapiga hatua kubwa kiuchumi na uchumi wa mwananchi mmoja mmoja utakua," alisema Lijualikali.


Alishauri serikali kujenga barabara za kiwango cha lami kuunganisha na stesheni za reli mpya ya kisasa.“Mradi huu utapendeza kama zitajengwa na barabara za kiwango cha lami kwa ajili ya kuunganika na stesheni za reli, hivyo kurahisisha maisha ya watu," alisema.