Home | Terms & Conditions | Help

November 30, 2024, 6:30 am

NEWS: KIPINDUPINDU CHAUWA WATU 12 NCHINI NIGERIA

LAGOS: Watu kumi na wawili wamefariki dunia kutokana na mlipuko wa maradhi ya Kipindupindu katika jimbo la Adamawa, Kaskazini-Mashariki mwa Nigeria, waziri wa afya wa jimbo hilo amesema.

Mlipuko huu mpya, ulioanza siku ya Jumapili, umeathiri watu 142 katika wilaya ya Mubi, Ahmad Sajo ameliambia shirika la habari la AFP.

"Tumeorodhesha vifo 12 kutokana na mlipuko wa maradhi ya Kipindupindu katika wilaya ya Mubi Kaskazini na Mubi Kusini kwa muda wa siku nne zilizopita," Waziri Sajo amesema.

"Jumla ya watu 142 waliambukizwa na timu za matabibu zimetumwa kuhudumia watu hao ambao tayari wameshaambukizwa ili kudhibiti maambukizi ya haraka ya ugonjwa huo," ameomgeza.

Amesema kuwa timu za matabibu bado hazijagundua sababu ya ugonjwa huo. Ugonjwa wa Kipindupindu ambao unaambukia kwa njia ya matumizi ya maji yalijaa virusi vya ugonjwa huo husababisha kuhara, na watoto ndio wako hatari kubwa ya maambukizi.

Magonjwa yanayotokana na maji ni tishio la mara kwa mara kutokana na ukosefu wa vifaa vya usafi kwa mazingira na madimbwi ya maji yanayokaa kwa kipindi kirefu wakati wa msimu wa mvua nchini Nigeria.