- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: KIFO CHA MTOTO WA EDWARD SOKOINE NI UTATA MTUPU.
WAKATI familia ya hayati Waziri Mkuu, Edward Moringe Sokoine ikidai mtoto wao, Tumaini Sokoine (41) maarufu kwa jina la Kereto amepoteza maisha kwa kuanguka siyo kwa kuchomwa kisu na mkewe, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo amesema Tumaini amepigwa na watu wawili wanashikiliwa na polisi.
Kamanda Mkumbo alisema watuhumiwa wawili wanaodaiwa kumuua Kereto, wanashikiliwa na polisi na tukio hilo lilitokea juzi saa 3.30 usiku nyumbani kwa marehemu Monduli Juu mkoani Arusha, yaliko makazi yao. “Ni kweli mtoto wa tano wa mke mkubwa wa hayati Sokoine ameuawa juzi usiku na katika tukio hilo polisi tunawashikilia watu wawili na upelelezi bado unaendelea,” alieleza Kamanda Mkumbo alipozungumza na gazeti hili.
Alisema polisi walipofika eneo la tukio na kukuta mwili wa marehemu ukiwa na majeraha mbalimbali mwilini, hali inayoonesha dhahiri kulikuwa na ugomvi nyumbani hapo. Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Monduli na kwamba utafanyiwa uchunguzi muda wowote na watuhumiwa watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
Wakati Kamanda Mkumbo akieleza hayo, familia ya Sokoine imedai Kereto aliruka ukuta wa uzio wa nyumbani kwa mama yake mzazi, Naponi ambaye ni mke mkubwa wa hayati Sokoine, na kuanguka kisha kugonga kichwa na damu kuvuja kwenye ubongo na kusababisha mauti yake.
Akizungumza kwa niaba ya familia, Msemaji wa familia ya hayati Sokoine, Lembris Kipuyo alisema kwa simu jana kwamba wamesikitishwa na taarifa ambazo siyo rasmi kuwa Kereto aliuawa kwa kuchomwa kisu kwenye ugomvi na mke wake, Maria.
Akifafanua, alidai kijana huyo alitoka nyumbani kwake saa 3:30 usiku kwenda nyumbani kwa mama yake na baada ya kufika hapo, alikuta lango kuu limefungwa. Alidai mtoto huyo alikuwa amekunywa pombe na baada ya kukuta lango kuu limefungwa, alilazimika kuruka ukuta na kwa bahati mbaya, alianguka na kugonga kichwa chini, hali iliyosababisha damu kuvujia kwenye ubongo.
“Marehemu anaishi umbali wa mita 600 kutoka nyumbani kwa mama yake na juzi kwa bahati mbaya alikuwa amekunywa kidogo na akilewa huwa anakuwa mkorofi kwa hiyo hakuvuta subira ya kufunguliwa lango kuu,” alidai Kipuyo ambaye ni Mkuu wa wilaya mstaafu. Kwa mujibu wake, watu waliokuwa nyumbani hapo walisikia kishindo kikubwa kwenye lango kuu na walipokwenda kuangalia, walimkuta Kereto amelala chini akivuja damu nyingi kichwani.
Kutokana na hali hiyo, alisema walimkimbiza katika Kituo cha Afya cha Engwiki kilichopo karibu na nyumbani hapo ambako alipatiwa huduma ya kwanza. Alisema baada ya kupatiwa huduma ya kwanza, alikimbizwa katika Hosptali ya Wilaya ya Monduli na kwa bahati mbaya alipoteza maisha kabla ya kufika hospitalini hapo.
Edward Moringe Sokoine alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na alifariki dunia kwa ajali ya gari Aprili 12, 1984 eneo la Dakawa mkoani Morogoro. Aliacha wajane wawili ambao wamekuwa wakiishi nyumbani kwake Monduli Juu, ambako ndiko alikozikwa mbunge huyo wa zamani wa Jimbo la Monduli. Sokoine alikuwa mchapakazi hodari na alipambana kikamilifu na wala rushwa na wahujumu uchumi.
#habarileo