Home | Terms & Conditions | Help

November 30, 2024, 10:37 am

NEWS: KESI VIONGOZI WAKUU WA CHADEMA YANGURUMA MPAKA SAA 2 USIKU

Dar es Salaam. Kesi inayowakabili viongozi wakuu wa chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA ililazimika jana Mei 16 kuendeshwa mpaka usiku wa saa 2 za usiku katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kabla ya kuahirishwa hadi Juni 11 baada ya kutokea kwa ubishani kati ya mawakili wa chama hicho na mawakili wa serekali.

Kiini cha ubishani katika kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa saa nane mchana jana ni upande wa utetezi katika kesi hiyo kuwasilisha pingamizi nane ukiomba mashtaka yanayowakabili washtakiwa yafutwe kwa sababu yana upungufu kisheria. Wakili wa utetezi Peter Kibatala katika ombi mbadala aliomba iwapo Mahakama itashindwa kuifuta hati nzima ya mashtaka, basi iyafute ambayo yana upungufu kisheria. Amedai maelezo kwa shtaka la nne, tano, sita na la saba yanawachanganya washtakiwa na hawawezi kujitetea kikamilifu. Pia, mashtaka hayo amedai ili kufunguliwa kunahitaji ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ambayo haipo.

Kesi hiyo inawakabili ni Freeman Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa Chadema, washtakiwa wengine ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; naibu katibu mkuu wa chama hicho Zanzibar, Salum Mwalimu; na wa Bara ambaye pia ni mbunge wa Kibamba, John Mnyika. Wengine ni mbunge wa Tarime Mjini Esther Matiko; katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji; mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; mbunge wa Kawe, Halima Mdee na wa Bunda, Ester Bulaya.

Image result for kesi ya viongozi wa chadema mahakamani

Wakili Kibatala aliwasilisha pingamizi hizo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi kuiambia Mahakama kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali na walikuwa tayari kwa kufanya hivyo. Nchimbi baada ya kueleza hayo, Kibatala alisema ni kweli lakini wamewasilisha pingamizi hizo za kisheria. Kibatala alidai panapokuwa na pingamizi kwa mujibu wa sheria ni lazima lisikilizwe kwanza. Upande wa mashtaka haukupinga na mahakama iliridhia

Image result for kesi ya viongozi wa chadema mahakamani

“Siyo kazi ya Mahakama kutafuta mashtaka yanayohusiana na hicho kibali cha DPP, hivyo hoja yetu hakuna ridhaa ya DPP kwa sababu kibali hicho si sahihi,” alidai Kibatala. Alidai shtaka la nne, tano, sita na saba kufunguliwa kwake kunahitaji ridhaa ya DPP na kwa kuwa haipo aliomba yafutiliwe mbali.

Kibatala alidai hati ya mashtaka ina upungufu kwa sababu shtaka la pili na la tatu hayana maelezo ya kutosheleza ya kuwapa msingi na uwezo washtakiwa kujitetea kikamilifu kijinai. Alidai katika shtaka la kufanya mkusanyiko bila kibali aliwataja hata watu waliotishiwa na kwamba wametajwa kwa wingi hivyo haijulikani ni washtakiwa au ni watu wengine.

Kibatala alidai mashtaka yanayowakabili wateja wake yamejichanganya, hayaonyeshi walisababishaje kifo cha Akwilina Akwilini, aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na majeruhi walijeruhiwa na nani na kwa kutumia nini. “Maelezo ya shtaka yamerundika vitu vingi kiasi kwamba ni vigumu mtu kujitetea na kwamba unapomshtaki mtu kwa kusababisha kifo ni lazima utoe maelezo ya kutosha kuonyesha unamaanisha kitu fulani ili mtu aweze kujitetea,” alidai.

Alidai hati ya mashtaka ina upungufu kwa kuwa haionyeshi dhumuni la pamoja ambalo washtakiwa walikutana kulitenda hivyo linawanyang’anya haki ya kujitetea. Alidai pia kuna upungufu wa kisheria kwa kuwa mashtaka hayaonyeshi watu waliochochewa kufanya makosa ni kina nani waliohudhuria mkutano, wakazi wa Kinondoni au wapigakura bila kujali itikadi zao. Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi alipinga hoja hizo za utetezi na kuiomba Mahakama itupilie mbali pingamizi hizo.