Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 5:33 pm

NEWS: KAMATI YA PAC YALAANI KITENDO CHA JESHI LA POLISI KUKAMATA WAANDISHI.

DODOMA: Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imelaani kitendo cha jeshi la polisi mkoani Dodoma, kumhoji kwa zaidi ya Saa tatu Mwandishi wa Habari wa gazeti la Nipashe, Augusta Njoji, kwa kuandika habari zilizotokana na vikao vya kamati hiyo.

Njoji alikamatwa juzi na Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Giles Muroto, akitakiwa kueleza masuala mbalimbali kuhusiana habari alizoandika ikiwamo kutaja majina ya wabunge waliyoibua hoja husika.

Habari hizo ni zinazohusu kashfa zinazogubika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ikiwemo ile inayohusu ununuzi na ufungaji wa vifaa vya utambuzi wa waharifu, kwenye vituo vyote vya jeshi hilo nchini, zabuni ambayo ilitolewa kwa Kampuni ya Lugumi Interprises.

Akizungumza na vyombo vya habari kwenye ukumbi wa Pius Msekwa, mjini hapa jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Naghenjwa Kaboyoka, amesema tukio hilo linamaanisha mhimili mmoja kuingilia mwingine kwakuwa habari iliyotolewa na mwandishi haina makosa yoyote.

“Kilichoandikwa na mwandishi huyu ni sahihi kabisa ndicho kilichozungumzwa kwenye kamati hivyo kumhoji na kutaka ataje walioibua hoja hizi, ni kutisha wanahabari waopelekea umma kazi zinazofanywa na wabunge ambao ni mhimili mwingine,”ameeleza mwenyekiti huyo.

Amesema tayari kamati hiyo imemuandikia barua Spika wa Bunge, Job Ndugai, ambaye kwasasa yupo nje ya nchi ili afanyie kazi suala hilo na kulitolea tamko ili ifike mahali mihimili iheshimiane.

Kaboyoka, amesema mara baada ya kupata taarifa za tukio hilo juzi, uongozi wa kamati hiyo ulikwenda kuzungumza na Kamanda Muroto ambaye alifikia maamuzi ya kufuta shauri hilo lililokuwa limefunguliwa dhidi ya Njoji, ambaye mpaka wakati huo alikuwa nje kwa dhamana.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa HabariMkoa wa Dodoma (CPC), Habel Chidawali, leo ametoa taarifa kwa vyombo vya habari kwamba uongozi wa chama hicho umezungumza na uongozi wa mkoa wa jeshi hilo, akiwemo kamanda Muroto, ambaye alikiri kwamba hawakutenda sawasawa.

Kupitia taarifa hiyo, Chidawali, ameeleza kuwa kamanda Muroto anaandaa mkutano na waandishi wa habari ili kuhakikisha uhusiano mzuri uliyokuwepo baina ya pande hizo mbili hauingii hitirafu.

Amewasihi waandishi wa habari nchini kuchukulia tukio hilo kuwa ni moja ya changamoto, hivyo kuruhusu hali ya maelewano kurejea katika kawaida kwa lengo la kutumikia Watanzania.