Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 9:49 pm

NEWS: JPM, SHEIN WAPITISHWA KAMATI KUU, NEC CCM.

DODOMA: Wakati Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ukianza leo na kuhitimishwa kesho mjini Dodoma, tayari chama hicho kimeazimia kwa pamoja kuwateua na kuwapitisha wagombea nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk John Magufuli kutetea nafasi yake na nafasi ya Makamu mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein wakati pia kimempitisha Philip Mangula kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole alisema katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM pamoja na mambo mengine, pia kimepitisha ajenda za mkutano mkuu wa taifa wa CCM.

“Leo (jana) vikao viwili vimeketi ikiwa ni pamoja na Kamati Kuu ya CCM (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (Nec) na vimefanya uteuzi na kuwapitisha wana CCM ambao wataomba ridhaa ya Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM kwa dhamana ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wake wa Bara na Zanzibar,” alisema Polepole. Hata hivyo, Polepole alieleza mkutano huo ni wa kawaida na unaoanzisha awamu ya uongozi wa CCM mpya ambao watakaa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2017 hadi 2022.

“Vikao hivi vimejadili, vimetafakari na kutoa mapendekezo ya ajenda za mkutano mkuu na pia vimetoa mapendekezo ya wana CCM ambao wanaomba dhamana hizi,” alisema. Alisema viongozi hao wanachaguliwa kwa mujibu wa Katiba ya CCM ibara ya 102(12) (a) ambacho kinaelekeza NEC kuteua majina ya wanachama watakaogombea wa nafasi hizo.

Katika mkutano huo, Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Salim Ahmed Salim alitoa neno la shukrani kwa utumishi wake wa miaka mitano 2012 hadi 2017 ndani ya CCM na kipekee alitoa shukrani kwa Rais Magufuli kwa uongozi mzuri, madhubuti na unaoweka mbele maslahi ya Watanzania hasa wanyonge.

Salim alibainisha kuwa Rais Magufuli amekuwa kielelezo tosha na kwa vitendo anaishi maisha yanayomuenzi baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere na atadumu kuhakikisha CCM inaimarika kwa manufaa ya amani na Umoja wa CCM na taifa la Tanzania. Wajumbe wa halmashauri Kuu Akizungumzia kwa upande wa uchaguzi wa wajumbe wa halmashauri kuu, Polepole alisema waliojitokeza ni zaidi ya 50 na kwenye kinyang’anyiro hicho, wajumbe 15 ndiyo watakaochaguliwa.

“2017 umekuwa mwaka wa uchaguzi, chama kimejitoa kwa faida ya Watanzania wakati huu tumekuwa na mwitikio mkubwa kwa Watanzania kugombea nafasi mbalimbali nchi nzima,” alisema.

Alisema tangu Aprili mwaka huu, wanachama zaidi ya 3,000 waliomba dhamana ya kugombea katika chaguzi mbalimbali za chama zilizofanyika nchi nzima. “Ngazi ya Taifa CCM tumepata mgombea mmoja nafasi ya Mwenyekiti nadhani ni tofauti na vyama vingine, na pia mgombea mmoja nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara, pia Zanzibar mgombea mmoja,” alisema Kwa upande wa mikoa, nafasi zilizogombewa ambazo tayari viongozi wake wameshapatikana ni Mwenyekiti CCM mkoa, nafasi ya ujumbe wa NEC Taifa kupitia mkoa, Katibu wa siasa na uenezi na nafasi mbalimbali zilizowaniwa kwenye jumuiya za chama hicho ambazo ni Umoja wa Wazazi, Umoja wa wanawake (UWT) na Umoja wa Vijana (UVCCM). Mkutano utahudhuriwa na viongozi wakuu wa CCM, viongozi wastaafu, viongozi mbalimbali katika chama na serikali.