Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 11:48 pm

NEWS : JESHI LA SYRIA LAFANIKIWA KUUKOMBOA MJI WA DEIR-EZ-ZOR

Jeshi la Syria laukomboa mji wa Deir ez-Zor, magaidi wa ISIS watimuliwa

Jeshi la Syria laukomboa mji wa Deir ez-Zor, magaidi wa ISIS watimuliwa

Jeshi la Syria limefanikiwa kuchukua udhibiti kamili wa mji wa Deir ez-Zor mashariki mwa nchi na kuwatimua kabisa magaidi wakufurishaji wa ISIS waliouteka mji huo mwaka 2014.

Jeshi la Syria limetoa taarifa leo asubuhi kupitia televisheni ya kitaifa na kusema "Mji wa Deir ez-Zor umekombolewa kikamilifu kutoka kwa magaidi."

Taarifa zinasema idadi kubwa ya magaidi wa ISIS wakiwemo makamanda wa ngazi za juu wameuawa katika oparesheni ya kuchukua udhibiti wa mji huo. Aidha Jeshi la Syria limeweza kunasa idadi kubwa ya silaha zilizokuwa katika maghala ya ISIS.

Deir ez-Zor ni mji mkuu wa mkoa Deir-ez-Zor wenye utajiri mkubwa wa mafuta na ambao unapakana na Iraq. Mji huo ulikuwa ngome kuu ya mwisho ya ISIS nchini Syria baada ya magaidi hao wakufurishaji kufurushwa mjini Raqqah, uliokuwa mji mkuu wao, kufuatia oparesheni ya wanamgambo wa Kikurdi wanaopata himaya ya Marekani.

Katika upande wa pili wa mpaka, Jeshi la Iraq lilitangaza Ijumaa kuwa limeanzisha oparesheni ya mwisho ya kuwatimua magaidi wa ISIS kutoka katika mji wa al-Qaim ulio katika mpaka na Syria. Mji huo pia unahesabiwa kuwa ngome ya mwisho ya magaidi wa ISIS nchini Iraq.

Kufuatia oparesheni hizo za majeshi ya Iraq na Syria, magaidi wa ISIS sasa hawatakuwa na ardhi wanazoshikilia katika nchi hizo na hivyo kuashiria kusambaratika kikamilifu 'khilafa' au dola bandia lililokuwa limetangazwa na magaidi hao wakufurishaji.