Home | Terms & Conditions | Help

November 30, 2024, 6:38 am

NEWS: JESHI LA POLISI LAJA NA OPERESHENI YA KUWASWEKA NDANI MADEREVA

JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, limezindua operesheni 'Nyakua Nyakua' ambayo itahusisha kuwakamata madereva wanaofanya makosa, kuwaweka mahabusu kabla ya kufikishwa mahakamani.

Kwenye operesheni hiyo, askari wa usalama barabarani hawatawatoza faini madereva watakaokutwa na makosa ikiwamo kuzidisha mwendo na badala yake watawaweka mahabusu na kisha kuwafikisha mahakamani siku inayofuata.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Fortunatus Musilimu, alisema jana May 23 kuwa, operesheni hiyo inafanyika kwa kuondoa mipaka ya kimikoa ambapo sasa askari wa kikosi hicho watakuwa wakishirikiana kukamata madereva wasiotii sheria.

"Tumegundua kuwa hii faini wana uwezo wa kuilipa ndiyo maana wanafanya makosa kwa kuamini kuwa watalipa," alisema Kamanda Musilimu. "Sasa hakuna kuwaandikia faini tena.
"Dereva akizidisha mwendo (trafiki) wamnyakue, weka ndani, peleka mahakamani."
Kamanda Musilimu alisema katika uzinduzi wa operesheni hiyo Mkoa wa Pwani waliwakamata madereva 40 ambao wamepatiwa mafunzo ya wiki mbili na maelekezo maalum, ili wakawe mabalozi kwa wenzao.

"Jana (juzi) nilikuwa mkoa wa Pwani kuzindua operesheni hii na kuna madereva 40 walikamatwa, lakini wamepewa mafunzo na nimewapa maelekezo maalum ya kufuata sheria za usalama barabarani endapo watakamatwa tena watafikishwa mahakamani," alisema.

"Ulipaji wa faini umewafanya madereva kurudia makosa hayo hayo kila siku," alisema.

Alisema madereva walio wengi wamekuwa wakitii sheria nyakati za mchana, lakini inapofika usiku wamekuwa wakiendesha magari yao kasi na kusababisha ajali.

"Ninazunguka mikoani na ujumbe kwa madereva ni kwamba kikosi cha usalama barabarani hakijalala, iwe usiku au mchana yeyote atakayevunja sheria hatua zitachukuliwa, jana (juzi) nilikuwa Pwani nimewaeleza hivyo madereva."

Alisema makosa yote ambayo ni vyanzo vya ajali za barabarani hayatakuwa na faini kama ilivyokuwa awali.

"Operesheni hii itafanyika kwa kuiunganisha mikoa mfano Iringa na Morogoro wanaungana, sasa hivi tunaelekea Tanga hivyo Mkoa wa Tanga na Pwani inaungana trafiki wa mikoa hii hawana mipaka tena ya kukamata," alisema.

"Nimeshakwenda Morogoro, Iringa, Manyoni, Igunga, Singida, Tabora, Pwani na sasa naelekea Tanga na baadaye Kilimanjaro na Arusha, tunaangalia ile mikoa yenye ajali sana ndipo tunatoa maelekezo."

Kamanda Musilimu alisisitiza kuwa kuanzia sasa madereva wasiofuata sheria za usalama barabarani watanyakuliwa kama mwewe anavyonyakua kifaranga lengo ikiwa ni kudhibiti ajali.

Chanzo Nipashe