Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 8:54 pm

News: Jafo atoa mwezi mmoja kufanya uchambuzi wa ubadhilifu wa mapato Hanang

MANYARA: Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Mhe. Selemani Jafo amemuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Hanang kuunda timu ya wataalam kuchunguza tuhuma za ubadhilifu wa mapato ya ndani yanayotokana na ushuru wa mazao.

Ametoa maelekezo hayo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani na Wataalam wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang kilichofanyika leo katika ukumbu wa mikutano wa Halmashauri hiyo, Mkoani Manyara

Mhe. Jafo ameutaka uongozi huo wa Wilaya kufanya uchunguzi kwa kuhusisha mchakato uliotumika kumpata mzabuni, ushiriki wa viongozi wa kisiasa katika mchakato huo, kubainisha mazingira ya rushwa kwa timu iliyofanya tathmini mwenendo mzima wa mapato na matumizi wa fedha za mapato ya ndani, mwenendo wa utendaji na ufanisi wa mashine za POS.

Ametoa maelekezo hayo baada ya kupatiwa taarifa za tuhuma za malalamiko juu ya kuwepo kwa migongano na mgawanyiko wa baraza la madiwani yasiyo na maslahi kwa wananchi.

Mhe. Jafo anaendelea kufafanua kuwa tuhuma zimeonyesha kuna harufu ya rushwa kwenye mchakato wa kumpata mkandarasi na baadhi ya viongozi wakubwa wa Halmashauri hiyo wanatajwa kunufaika kwa kupewa fedha takriban mil 1.5 kila mwezi suala hili halikubaliki katika utendaji kazi wa sasa.

Amemulekeza Mkuu wa Wilaya kuunda timu ya kufuatilia tuhuma hizo iliukweli ubainishwe, taarifa iwasilishwe Mkoani kisha Wizarani ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya wabadhilifu hao.

Ameelekeza kuwa kuimarishwa kwa ushirikiano na mahusiano miongoni mwa viongozi, madiwani, na wataalam ili kuleta maendeleo kwa wananchi na kuacha migongano ambayo haina maslahi kwa wananchi.

Mhe. Jafo amewaasa wanasiasa kuacha tabia ya kujihusisha na majukumu ya kitaalam badala yake wasimamie utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya halmashauri yao kwa faida ya wanachi waliowatuma kazi

”Wanasiasa acheni kuujihusisha na majukumu ya kitaaluma badala yake simamieni utekelezaji wa mipango ya maendeleo katika Halmashauri ili kuwasaidia wananchi” Alisistiza Jafo.

Mhe. Jafo amesisitiza kuwa watanzania wanaimani kubwa sana na serikali yao ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania hivyo inashangaza kuona baadhi ya viongozi wa kisiasa na wataalam kutokuwa na huruma na wanachi wao waliowatuma kuwatumikia kupitia ilani ya uchaguzi ya CCM 2015-2020

Amesema Serikali imejipanga kuleta mabadiliko makubwa sana kwa kutoa huduma bora na za uhakika kwa wananchi, hivyo watumishi wa umma kuwa chachu ya mabadiliko hasa ikizingatia kuwa zaidi ya watumishi, hivyo wanapaswa kuwahudumia wananchi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe Alexander Mnyeti aliunga mkono kauli ya Waziri kuhusu hujuma na michezo michafu ya wanasiasa wa Hanang inayosababisha kurudisha nyuma maendeleo ya Halmashauri hiyo.

Aidha Mkuu wa Mkoa huo ameishukuru TAMISEMI kwa kumteua Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ambaye ni jasiri, mchapa kazi, muwazi na hapendi kupindisha mambo kinyume na sheria, taratibu na kanuni.