Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 7:40 pm

NEWS: JAFO AKUNWA NA UJENZI WA MIRADI MVOMERO

MVOMERO: Waziri wa Nchi, ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi)Selemani Jafo amewapongeza viongozi na watendaji wa wilaya na Halmashauri ya wilaya ya Mvomero kwa usimamizi wa Miradi ya maendeleo.

Jafo aliyasema hayo alipokuwa ziarani wilayani huko ambapo alifanikiwa kutembelea ujenzi wa hospitali ya wilaya, shule ya kidato cha tano na sita ya kumbukumbu ya Sokoine, mradi wa ujenzi wa barabara ya lami, kituo cha mafunzo ya kilimo na mifugo, pamoja na mradi wa umwagiliaji.

Katika ziara hiyo,Jafo ameagiza kuanza kwa utoaji wa huduma ya matibabu kwa wagonjwa katika hospitali ya wilaya ya Mvomero ifikapo keshokutwa Desemba 13,mwaka huu wakati serikali ikitafuta fedha kwaajili ya ujenzi wa jengo la upasuaji, maabara, wodi ya watoto na majengo mengine ambayo yatagharibu zaidi ya sh.milioni 700 ambapo matarajio ni kupata fedha hizo na kukamilisha majengo hayo kabla mwezi Machi 2018.

Pia Jafo ameagiza kuongezeka kwa kasi ya kukamilisha madarasa, bwalo la chakula na mabweni katika shule ya sekondari ya Sokoine Memorial kabla mwezi April 2018 ili shule hiyo iweze kupokea wanafunzi wa kidato cha tano hapo mwakani kwani serikali imepeleka fedha zote za ujenzi zaidi ya sh.billioni 1.6.

Aidha Jafo amewataka viongozi na watendaji kuendelea kushikamana ili kuwaletea wananchi maendeleo.