Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 1:43 pm

NEWS: JAFO AKERWA NA UCHAFU WA MAZINGIRA BAGAMOYO MJINI.

BAGAMOYO: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)Selemani Jafo ameonyesha kukerwa sana na uchafu wa mazingira katika kituo cha mabasi pamoja na mifereji ya barabara ndani ya mji wa Bagamoyo.

Hali hiyo imejitokeza leo katika ziara yake ya kikazi wilayani humo.

Akiwa katika kituo cha mabasi ameshangazwa na vyoo vya kituo hicho kuonekana vimefungwa mara kwa mara na kusababisha madereva pamoja na abiria kujisaidia katika maeneo yasiyo rasmi.

Hali hiyo imesababisha mkojo na vinyesi kutapakaa katika mifuko ya lambo iliyofungwa na kutupwa nyuma ya vibanda vya biashara vinavyozunguka kituo hicho.

Pia Waziri Jafo ameshuhudia kutapakaa kwa uchafu katika mifereji ya barabara mbele ya nyumba za watu ambapo amedai kitendo hicho kinaonesha kwamba hata wakazi hawasimamiwi katika kusafisha maeneo ya mbele ya nyumba zao.

Kufuatia hali hiyo, Jafo ameutaka uongozi wa Halmashauri hiyo kubadilisha hali iliyopo sasa na kumuagiza Afisa Afya na Afisa Mazingira kujieleza ndani ya siku mbili kwanini wasichukuliwe hatua kwa kushindwa kutimiza majukumu yao.

Wakati huo huo, Waziri Jafo ametoa mwezi mmoja kwa halmashauri hiyo kukamilisha ufungaji wa mfumo wa ukusanyaji wa mapato ujulikanao kwa jina na GoTHoMIS katika hospitali ya wilaya hiyo