Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 3:20 am

NEWS: IRAN YAANZA KUFANYA BIASHARA NA MATAIFA YA ULAYA

Taifa la Iran na Umoja wa Ulaya hatimaye zimekamilisha mauziano ya kwanza chini ya mfumo wa ubadilishanaji ws bidhaa na huduma uliowekwa ili kukikiuka vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu.

Nchi za Ujerumani, Ufaransa na Uingereza zimefanya mauzo ya mwanzo kabisa kwa kutumia mfumo wa kubadilishana bidhaa uliowekwa ili kuvikwepa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, na mataifa hayo ya Ulaya yameweza kutuma vifaa vya matibabu kwenye taifa hilo la Kiislamu.

Taarifa iliyotolewa jana na wizara ya mambo ya kigeni ya Ujerumani inasema kwamba hatua hiyo ni matokeo ya majaribio ya muda mrefu ya Ulaya kuuzindua mpango huo uitwao INSTEX, ambao unahusisha biashara halali na Iran licha ya kuwepo vikwazo vya Marekani.

Ofisi hiyo ya mambo ya kigeni ya Ujerumani imesema kuwa bidhaa hizo tayari zimewasili Iran, ikiongeza kuwa mfumo huo wa INSTEX utatumika pia kwenye mauziano mengine na mfumo kama huo wa upande wa Iran uitwao STFI.

Mfumo huo ulibuniwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita baada ya Marekani kurejesha upya vikwazo vikali dhidi ya sekta ya mafuta ya Iran kufuatia hatua ya Rais Trump kujiondowa kwenye makubaliano ya kimataifa kati ya Iran na mataifa sita yenye nguvu duniani juu ya mpango wake nyuklia.