Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 11:44 am

NEWS : INTERPOL YAWANASA WATU 40 KWA KOSA LA KUFANYA MAGENDO YA BINADAMU NCHINI LIBYA

Interpol yawatia nguvuni watu 40 kwa kufanya magendo ya binadamu Libya

Interpol yawatia nguvuni watu 40 kwa kufanya magendo ya binadamu Libya

Watu wasiopungua 40 wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kufanya magendo ya binadamu katika eneo la magharibi mwa Afrika baada ya kusambaa mkanda wa video unaoonesha wakimbizi wa Kiafrika wakipigwa mnada na kuuzwa kama bidhaa nchini Libya.

Katika taarifa yake ya jana Alkhamisi, Polisi wa Kimataifa wa Interpol imesema, watu waliotiwa mbaroni wanakabiliwa na mashtaka ya uhalifu ikiwemo kufanya magendo ya binadamu, kufanyisha watu kazi kwa lazima na kuwatumia vibaya watoto wadogo. Interpol imesema pia kuwa, takriban watu 500 wakiwemo 236 wenye umri mdogo wameokolewa katika opereseheni zilizofanyika kwa wakati mmoja katika nchi za Chad, Mali, Mauritania, Niger na Senegal.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Opereseheni hizo za Interpol zimefanyika baada ya dunia kukasirishwa na mkanda wa video uliowaonesha Waafrika wakipigwa mnada na kuuzwa kama watumwa nchini Lbiya. Wiki iliyopita, televisheni ya CNN ilirusha hewani mubashara mnada wa kuuza Waafrika huko nchini Libya ambapo kila mtu alikuwa akiuzwa kwa dola zisizopungua 400 za Kimarekani. Wamiliki wa mashamba ndio waliokuwa wanunuzi wakuu wa "watumwa" hao katika mnada huo.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema hivi karibuni kwamba mnada huo wa kuwauza Waafrika kama watumwa nchini Libya ni uhalifu dhidi ya binadamu.

Libya ilitumbukia kwenye machafuko tangu mwaka 2011 baada ya madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani kuingia kijeshi huko Libya katika kampeni ya kumng'oa madarakani Kanali Muammar Gaddafi. Tangu mwaka huo hadi hivi sasa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika haijawahi kushuhudia usalama na utulivu hata mara moja.