- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: IGP, MAKAMANDA WA POLISI WAPEWA AGIZO.
DOM: Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro, Makamanda wa Polisi wa Mikoa na vikosi, wameagizwa kuwachukulia hatua za kinidhamu askari wanaotumia nguvu kupita kiasi, kunyanyasa raia na kuendekeza vitendo vya rushwa.
Agizo hilo limetolewa leo jijini hapa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Logola, kwenye hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kwenye wizara hiyo, Issa Ngimba, wakati akifungua mafunzo ya maofisa wa ngazi za juu wa jeshi hilo.
“Mafunzo haya yataongeza viwango na ubora wa utendajikazi kwa maofisa wa ngazi za juu wa polisi. Hata hivyo wapo baadhi ya askari wanaoendekeza rushwa, matumizi ya nguvu kupita kiasi na unyanyasaji wa kijinsia.
“IGP pamoja na makamanda wa polisi wa mikoa, mnapaswa kuwachukulia hatua askari hao,” amesisitiza.
Hata hiyo ameongeza kuwa watumishi wa jeshi hilo wanatakiwa kuwa na uelewa wa pamoja bila kujali tofauti za vyeo vyao, katika kuwatumikia wananchi.
Awali kabla ya hotuba hiyo, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Profesa Joseph Semboja, amesema polisi ndio sura ya serikali kwani mara nyingi ndio wamekuwa wakikutana na jamii.
“Kwa sababu hiyo, utendaji mzuri wa polisi ndio sifa nzuri kwa serikali,” amebainisha.
Profesa Semboja ameeleza kuwa mafunzo hayo yanayotolewa na Taasisi ya Uongozi, yanalenga kuongeza ujuzi, maarifa na uelewa wa polisi katika kutimiza majukumu yao.
“Wakati taasisi inaanzishwa miaka minane iliyopita, hatukutegemea kuwa polisi watakuwa wadau wetu.
“Mmoja kati ya wajumbe alikwenda kuonana na rais (Dk. John Magufuli), katika mazungumzo yao alipewa maagizo kuwa Taasisi ya Uongozi kwenye mafunzo yake inapaswa kuzizingatia taasisi tatu moja wapo ikiwa polisi,” amefafanua.
Naye Mkuu wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu kwenye Jeshi la Polisi, Alfred Nyamhanga, ameeleza matukio ya uhalifu kwa mwaka huu yamepungua kwa asilimia 13.7.
Ameeleza kuwa dhima ya jeshi hilo ni kutoa huduma bora za usalama wa raia kwa kubaini na kudhibiti matukio ya kiharifu.
Kamishna huyo wa polisi, amesema katika kufanikisha dhima hiyo polisi wanapaswa kufanyakazi kwa nidhamu, uzalendo, kujifunza, ubunifu, utiifu, uadilifu na uvumilivu.