Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 12:39 am

NEWS: HAONGA AWASHUKIA WABUNGE WANAOHAMIA CCM.

Mbunge wa Mbozi (Chadema) Pascal Haonga amesema watu walioaminiwa na kuchaguliwa wakiwa upinzani na kuhamia CCM uwezo wao wa akili unapungua.


Akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2019/20 jana Alhamisi Novemba 8, 2018, Haonga alisema kuna mbunge mmoja (Mbunge wa Ukonga-CCM Mwita Waitara) amesema kuwa aliondoka Chadema sasa yupo huru CCM.


“Alisema kuwa ameondoka kwa sababu alitaka kugombea uenyekiti na Mbowe (Freeman Mbowe- Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani BUngeni) lakini akakataliwa sasa yuko huko tuone kama ataenda kugombea uenyekiti na mheshimiwa Magufuli (Rais John Magufuli) na atakubaliwa,” alisema Haonga.


Alisema wananchi wanategemea mtu akichaguliwa atimize miaka mitano ndipo aombe kuchaguliwa tena lakini si hivyo hivi sasa fedha zinazotumika kwa ajili ya uchaguzi ni nyingi.


Alisema fedha hizo zingeweza kwenda katika miradi ya maendeleo zingesaidia kukamilisha miradi ya barabara, shule na zahanati nchini.


Hata hivyo, Mbunge wa Kinondoni (CCM) Maulid Mtulia alimpa taarifa mbunge huyo kuwa hakutakuwa na upotevu wa fedha akitoka upinzani akienda CCM atapita bila kupingwa na kwamba limeshaanza kufanyiwa kazi.


Kauli iliyopokelewa na Spika wa Bunge Job Ndugai, “Taarifa hiyo mheshimiwa Haonga tena linateleza tu.”


“Siku zote kama ulikuwa katika chama ambacho watu walikuamini na wakakuchagua katika chama hicho ni lazima ukihamia chama cha CCM lazima uwezo wako wa akili utapungua,” alisema Haonga baada ya Ndugai kumalizia kuzungumza.


Hata hivyo, Spika Ndugai alimjibu kuwa kauli hiyo si ya kibunge na ni ya dharau kwa watu wengine.


“Usifike mahali pa kuwafanya watu kama watoto, hawa ni watu wazima wamefanya decision (ni maamuzi) yao you have to respect others dicision (unatakiwa kuheshimu maamuzi yao),”alisema.


Alimtaka kutoendelea lugha hiyo bali aendelee kuchangia mapendekezo hayo, kauli ambayo Haonga alikubaliana nayo.