Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 8:37 pm

NEWS: HALIMA MDEE AFUNGUKA ADAI HAJAWAHI KUONA BUNGE LINAPELEKWA NA SERIKALI.

BUNGENI DOM: September 4, 2018 Wabunge walikuwa wakijadili Muswada wa sheria ya kulitangaza jiji la Dodoma kuwa makao makuu ya nchi wa mwaka 2018 (The Dodoma capital city Declaration Bill 2018) ambapo miongoni mwa waliopata nafasi ya kuchangia ni pamoja na Mbunge wa Kawe Halima Mdee ambaye amekosoa taratibu zilizotumika na Serikali katika kutekeleza mapendekezo hayo.

Amesema hakuna anayepinga Dodoma kuwa jiji wala Serikali kuhamia lakini hoja ni utaratibu wa kisheria umekiukwa na pia mipango ya Taifa haijatekelezwa kama Katiba inavyotaka.


“Isije ikajengwa propaganda kwamba kuna mtu anapinga Dodoma kuwa makao makuu maana sasa hivi siasa zetu zimetoka katika hoja na kwenda katika vihoja,”amesema.


Mdee ambaye pia ni mwenyekiti wa baraza la wanawake wa Chadema (Bawacha) amesema Serikali imechomeka suala la makao makuu na hivyo kuhalalisha Bunge kupokonywa mamlaka yake kisheria.


“Mimi nimekuwa mbunge kwa awamu tatu, mara ya kwanza nikiwa mbunge wa viti maalum na kisha mbunge wa jimbo kwa mara mbili, sijawahi kuona Bunge linalopelekwa pelekwa kama hili,” amesema Mdee.


Amesema anasheria ya mipango miji ya mwaka 2008 ambayo inaonyesha vigezo vya jiji ni pamoja na mamlaka ya kutangazwa kwa eneo kuwa jiji ni ya Bunge.


“Sasa mtuambie ni lini Bunge hili lililetewa muswada wa sheria ambao uliinyanyua Dodoma kuwa jiji,” amesema.


Amesema Rais John Magufuli hana mamlaka ya kulitangaza Dodoma na kwamba Rais anaweza kusema lakini ni mamlaka ya Bunge kulipa uhalali ya kuwa jiji lazima itekelezwe.


Amesema alitarajia waziri kusema wanaitambua Dodoma kuwa makao makuu lakini ndani yake wamechomekea kuhusu jiji kuna vigezo kadhaa vimefikiwa.


Amesema ni wajibu wa Spika Job Ndugai kulinda heshima na hadhi ya Bunge hilo.


Akijibu hoja hiyo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Adelardus Kilangi amesema wabunge wengi waliosema kuwa Rais alikosea kulitangaza Dodoma kuwa jiji walitumia Sheria ya Mipango Miji.


Amesema si sahihi kutumia sheria hiyo na kwamba sheria hiyo ilikusudiwa kwa ajili ya kuweka mipango mizuri ya matumizi ya ardhi katika maeneo ya mijini.


Amesema sheria sahihi ambayo Rais Magufuli aliitumia ni Sheria ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa ambayo inasema mamlaka ya kutangaza jiji yako kwa Rais.