Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 12:51 am

NEWS: HABARI NZURI KWA WANAWAKE WANAOTAKA KUPANDIKIZA MATITI

Dar es salaam: Hospitali mbili nchini Hospitali ya taifa Muhimbili na Aga khan zimeanzisha programu ya kufanya upasuaji wa upandikizaji wa Matiti, hii ni kwa wanawake wasio kuwa na matiti na wanawake wanaotaka kupunguza au kuongeza matiti, programu hii itawasaidia wanawake wasiokuwa na matiti baada ya kukatwa ili kutibiwa saratani ya matiti.

Akiongea Jana (3.11.2017) Bingwa wa Upasuaji wa Hospitali ya Aga Khan, Dk. Aidan Njau amesema kuwa madaktari wa Aga Khan watafanya upasuaji huo kwa kushirikiana na madaktari wenzao kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Shirika la Kimataifa lisilo la Serikali la Women for Women la nchini Marekani, alisema kuwa wanawake wawili tayari wameandaliwa kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji huo.

“Ni awamu ya tatu sasa tunafanya upasuaji kwa akina mama, watoto na mabinti waliopata madhara katika miili yao kutokana na ajali mbalimbali, lakini kwa upande wa upandikizaji matiti huu ni upasuaji wa kwanza tunaanza kufanya hapa nchini,” alisema na kuongeza:
“Tunachofanya ni kutengeneza viungo vyao ili virudi katika hali ya kawaida ili na wao waweze kuendelea na maisha yao kama watu wengine.


“Mara nyingi mtu anapoelezwa kuwa ana tatizo la saratani wengi huathirika kisaikolojia na mama anapofanyiwa upasuaji wa kuondoa titi kama sehemu ya matibabu dhidi ya saratani huzidi kuathirika kisaikolojia.
“Maumivu huongezeka pale anapoelezwa kuwa matibabu ni kuondolewa ziwa lake kama sehemu ya matibabu, hivyo tunaona upasuaji huu utawafaa na utawasaidia wengi ambao walipoteza kiungo hicho.
“Tunachofanya, tunachukua sehemu katika mwili wake na kutengeneza titi ambalo tutakuja kulipandikiza tena kwenye mwili wake, ingawa haitakuwa kama ziwa ambalo Mungu alimpatia, lakini litamwezesha kuwa kama wanawake wenza" alisema