Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 11:44 am

NEWS : DURU ZA MAZUNGUMZO YA AMANI YA BURUNDI KUANZA LEO MKOANI ARUSHA

Duru mpya ya mazungumzo ya Burundi kuanza leo Arusha, Tanzania

Duru mpya ya mazungumzo ya Burundi kuanza leo Arusha, Tanzania

Duru mpya ya mazungumzo ya amani ya Burundi inaanza leo Jumatatu mkoani Arusha, na itaendelea hadi Disemba 8.

Mazungumzo hayo yanaongozwa na Benjamin William Mkapa, Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni mpatanishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mgogoro wa kisiasa wa Burundi.

Muungano wa upinzani wa CNARED umesema hautashiriki katika mazungumzo hayo ukisisitiza kuwa, mpatanishi wa mgogoro huo Benjamin Mkapa amekuwa akiegemea upande wa serikali.

Wawakilishi wa serikali ya Burundi walikataa kushiriki mazungumzo ya moja kwa moja na wawakilishi wa CNARED katika mazungumzo yaliyopita, wakiwatuhumu kuhusika na jaribio lililofeli la mapinduzi dhidi ya serikali ya Rais Pierre Nkurunziza mnamo Mei 14, 2015.

Benjami Mkapa, rais mstaafu wa Tanzania

Burundi ilitumbukia katika machafuko mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka 2015 baada ya chama tawala cha CNDD-FDD kumuidhinisha Nkurunziza kugombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita kwa mara ya tatu mfululizo.

Wapinzani waliitaja hatua ya Rais Nkurunziza kushiriki katika uchaguzi huo kwamba ilikiuka katiba na hati ya makubaliano ya amani ya Arusha lakini serikali ya Bujumbura ilisema haijakiuka sheria.

Kwa mujibu wa mashirika mbali mbali ya haki za binadamu, watu zaidi ya elfu 2 wameuawa katika machafuko hayo, kiasi cha majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kuruhusu kuanzishwa uchunguzi kuhusu ukatili na jinai dhidi ya binadamu uliofanywa katika kipindi cha kati ya mwaka 2015 na 2017. Ifahamike kuwa, Burundi ilijiondoa kwenye Mkataba wa Roma uliounda mahakama hiyo ya mjini The Hague, Uholanzi.