- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: DED AINGIA MATATANI KWA UBADHIIFU WA MAMILIONI YA SHILINGI
BAHI DOM: Madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma wametuhumu Mkurugenzi wa wilaya hiyo Rachel Chuwa kwa kudai kuwa ni miongoni mwa watu waliohusika na ubadhirifu wa Mamilioni ya shilingi na kuagiza mamlaka ya uteuzi imchukulie hatua kali.
Pia fedha hizo zinadaiwa zimetumika kinyume na utaratibu kwa kujilipa posho kwa baadhi ya watumishi wa Halmashauri hiyo huku zikikosekana nyaraka za matumizi mbalimbali.
Akiwasilisha taarifa ya kamati ya ndogo iliyoundwa na Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango kwa niaba ya Mwenyekiti wa kamati hiyo Mathayo Malilo, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Sostenes Mpandu, alisema kamati hiyo iliundwa kwa mujibu wa sehemu ya IV kifungu cha 45(1)-(4) cha kanuni za kudumu za Halmashauri.
Amesema lengo la kamati hiyo ilikuwa ni kupitia matumizi ya fedha katika akaunti ya amana na mapato ya ndani baada ya kutokea sintofahamu ya fedha kwenye akaunti ya amana.
Amesema katika kazi hiyo kamati hiyo iliweza kupitia nyaraka mbalimbali zikiwemo ripoti ya Kamati ya fedha za kila mwezi kwa mwaka wa fedha 2015/16, 2016/17 na Julai 2017 hadi Machi 2018, taarifa za benki, kitabu cha malipo(cash book) na mahojiano ya baadhi ya watumishi wa halmashauri.
Akaunti ya amana
Akiendelea kueleza amesema kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai 2015 hadi Septemba 2017 kiasi cha Sh.Milioni 311.2 zilikuwa zimekopwa kwa kazi mbalimbali.
Amesema baada ya kamati kuchambua taratibu za fedha ilibaini kuwa kwenye akaunti hiyo katika kipindi cha Julai hadi Disemba 2015 kiasi cha Sh.Milioni 188.55 zilikopwa kupitia akaunti hiyo wakati Kikao cha wakuu wa Idara chini ya Mkurugenzi(CMT) ikiwa imekaimu majukumu ya kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango.
“Pia katika kipindi cha januari 2016 hadi septemba 2017 kiasi cha Sh.Milioni 106.84 zilikopwa kupitia akaunti ya amana, na kipindi hicho Sh.Milioni 30.5 ndizo zilizofuata utaratibu kwa kuidhinishwa na kamati ya fedha,”ameongeza kwa kusema Mlilo.
Licha ya hayo amesema maombi ya fedha Sh.Milioni 30.5 ambayo yalikuwa ya Kliniki tembezi na jumuiya ya watumiaji wa maji Kigwe, maombi yaliyofikishwa kwenye kamati husika wakati fedha kiasi cha Sh.Milioni 38.6 tayari zilikuwa zimekopwa na Okotoba 20, mwaka 2017 akaunti ilibaki na salio sifuri.
Kamati imebaini kuwa Mwekahazina wa wakati huo Ponsian Kilumbi aliweza kulipwa fedha za masomo ya CPA kiasi cha Sh.Milioni 3.9 kwa mwaka wa fedha 2015/16 kupitia fedha za amana ilihali Mweka hazina hakupitishwa na kamati ya fedha kama taratibu zinavyotaka na kutokuwepo kwenye mpango na bajeti ya Halmashauri kwa mwaka husika.
Amesema katika uhakiki wa matumizi ya akaunti hiyo kamati imebaini kuwa Dk.Rainer Kapinga aliyekuwa Mganga Mkuu wa wilaya(DMO) aliweza kulipwa kiasi cha Sh.Milioni 3.7 za akaunti hiyo kwa ajili ya pango na uhamisho kwa madai kuwa zitarudishwa kupitia fedha za matumizi mengineyo(OC) ya idara.
“Mnamo mwezi agosti 2015 kiasi cha Sh.Milioni 3.1 zililipwa kwa ajili ya vikao vya CMT vilivyoketi Februari 2014 hadi Machi 2015 malipo haya yalikuwa ni madai ya nyuma ambayo kiutaratibu yalipaswa yaletwe kama maombi kwenye kamati hiyo,”amesema.
Posho
Amesema kiasi cha Sh.Milioni 116.38 cha fedha za amana zilitumika kama posho zisizo na ulazima zikijumuisha masaa ya ziada Sh.Milioni 24.2 kufunga mahesabu ya mwaka Sh.Milioni 34.6, shughuli za nane nane Sh.Milioni 45.3 na shughuli za mwenge Sh.Milioni 12.1.
Udanganyifu wa taarifa
Katika ripoti ya kamati hiyo, alisema kamati imebaini fedha Sh.Milioni 51 walizolipa LIC zinazodaiwa kulipia kodi ya zuio Mamlaka ya Mapato(TRA), imebainika haikuhusika na ulipaji wa kodi hiyo badala yake malipo ya zuio imeonekana kulipwa na wakandarasi wenyewe kiasi cha Sh.Milioni 54.9 kwa Hati ya malipo namba 01286 ya Machi 18, mwaka 2017.
Athari za utekelezaji wa miradi
Amesema kuchukuliwa kwa fedha hizo za amana na kutorejeshwa kumesababisha halmashauri kudaiwa na wakandarasi au watoa huduma Sh.Milioni 250.
“Pia athari nyingine iliyojitokeza ni pamoja na Halmashauri kupata kusudio la kushitakiwa mahakamani kwa kusudio la kushitakiwa mahakamani kwa kusudio namba ELEG/Bahi/1/2018 kwa kutolipa fedha yake anayoidai Halmashauri Sh.Milioni 31.8 za mradi wa maji wa Mundemu-Nguji,”amesema.
Aidha amesema mradi wa usambazaji wa maji Mkakatika-Bahi zilibaki Sh.Milioni 17 kupitia Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP) na Sh.Milioni 32 zilizokuwa zifanye utafiti wa mradi wa maji Mbwasa-Bahi zilitokana na Sh.Milioni 100 zilizoletwa na Wizara ya maji kupitia Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira hazikutumika na hazipo kwenye akaunti.
Akaunti ya mapato ya ndani
Mpandu amesema kamati imebaini Sh.Milioni 2.84 kupitia hati ya malipo namba 00277 ya Agosti 30, mwaka 2017 zililipwa kwa wakuu wa idara kama posho ya kujikimu kusimamia kuweka alama za ng’ombe zoezi hilo halikufanyika.
Pia amesema kamati imebaini matumizi ya kiasi cha Sh.Milioni 2.3 kupitia hati ya malipo namba 00153 ya Agosti 17, mwaka 2017 zilitumika kama posho ya kuhamasisha upigaji chapa ng’ombe, kiasi cha Sh.390,000 kati ya hizo alizolipwa Mweka hazina Saad Shibailu hajawahi kwenda kuhamasisha hata siku moja.
“Kamati imebaini Sh.Milioni 3.06 kupitia Hati ya malipo namba 00277 ya agosti 30, mwaka 2017 zilitumika kujilipa posho za kujikimu za siku 18 ufuatiliaji wa ujenzi wa majengo kwa vijiji vitano watumishi hawakuonekana,”alisema.
Amesema kamati pia imebaini kiasi cha Sh.Milioni 1.79 kupitia hati ya malipo namba 00923 ya Novemba 17, mwaka 2017 zilitumika kulipa posho ya kujikimu ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ambapo Mkurugenzi, Mweka hazina, Afisa Mipango, Mchumi na Dereva hawakwenda kukagua.
“Mafunzo ya Tathmini ya wazi ya utendaji kazi(OPRAS) kiasi cha Sh.Milioni 1.98 kati ya Sh.Milioni 2.52 kimetumika kwa njia ya udanganyifu ambapo mafunzo yalifanyika siku tatu badala ya 14, na wahusika ni Afisa Rasilimali watu na utumishi wilaya(DHRO)Fauzia Nombo, Afisa Rasilimali watu na utumishi(HRO)Kawina Tawete na dereva,”amesema.
Pamoja na hayo, amesema hati ya malipo namba 1580 ya Sh.Milioni 1.75 yaliyolipwa kwa Mkurugenzi, DHRO, HRO na dereva kufanya kazi ya ukaguzi wa utendaji na taratibu za uendeshaji wa serikali za vijiji vya Makanda, Msisi, Kiwanja cha ndege, Tinai, Mundemu na Nguji haukuwahi kufanyika.
“Kiasi cha Sh.850,000 kupitia hati ya malipo namba 871 zililipwa kwa Barnabas Ngugo, Abella Mtembezi na dereva Idd Kagomba kama posho ya kujikimu kwa siku tano kwa ajili ya kufuatilia vitabu vya makusanyo, imebainika kazi hiyo haijawahi kufanyika,”amesema.
Aliongeza “Mkurugenzi(Rachel Chuwa) alilipwa 600,000 kwa kuhudhuria kikao cha Bodi ya ajira mwaka 2017 wakati wa kuajiri nafasi za watendaji wa vijiji wakati si mjumbe wa kikao na hakuwahi kuhudhuria,”.
Changamoto
Amesema hazikuonekana zenye thamani ya Sh.Milioni 136.06 kwenye akaunti ya amana na Sh.Milioni 225.421 kwenye akaunti ya mapato ya ndani ambazo kwenye mfumo wa EPICOR zimeweza kuonekana lakini vocha zake hazikuweza kupatikana.
Mapendekezo
Pamoja na mapendekezo hayo kwa mamlaka ya uteuzi pia imependekeza malipo ya udanganyifu yaliyofanyika wahusika warejeshe fedha hizo na watumishi waliotajwa kwenye ripoti ya kamati waandikiwe barua za onyo.
Kauli za madiwani
Wakichangia baada ya kuwasilishwa ripoti hiyo,Madiwani waliunga mkono mapendekezo ya kamati hiyo ndogo huku wakisema hatua hiyo itaifanya halmashauri kusonga mbele kimaendeleo.
Mwenyekiti wa Halmashauri
Kwa upande wakeMwenyekiti wa Halmashauri Danford Chisomi ameagiza kuanzia jana watumishi waliotajwa kwenye ripoti andikiwe barua za kurejesha fedha na za onyo huku akiwaonya watumishi wa wilaya hiyo kuwa madiwani hawatafumbia ubadhirifu wowote utakaofanywa.
Aidha amesema wanasubiri ripoti nyingine kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuhusu jambo hilo ambapo itatolewa ndani ya siku saba kuanzia jana.
“Nyaraka zote ambazo hazikupatikana zipatikane kwa kuwa tunajua zipo ziandaliwe na zikaguliwe,”amesisitiza.
Kauli ya Mkurugenzi
Akizungumzia tuhuma hizo,Mkurugenzi huyo amesema amesikiliza kwa makini tuhuma lakini zina kasoro kwa kuwa hakupewa nafasi ya kuzijibu kwenye kamati hiyo.
“Kwa bahati mbaya tangu walipomaliza ripoti yao tangu kikao cha Juni 26, mwaka huu, ikaenda kamati ya Fedha, mipango na uongozi na wakalichukua moja kwa moja kama ni kweli jambo hili limetendeka na wakachukua na kupeleka kwa Katibu Tawala wa Mkoa(RAS),”amesema.
Amesema ni vyema mtuhumiwa angepewa nafasi ya kujibu tuhuma zake kwenye kamati lakini suala hilo linaonekana lina sura ya kipekee huku akisisitiza kuwa tuhuma zilizotolewa hazina ukweli.