Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 8:51 am

NEWS: DART YADAI KUHUJUMIWA NA MADEREVA WAKE

Dar es Salaam: Kampuni ya usafirishaji wa Abiria ya magari yaendayo kasi (Udart) imetoa malalako yake kwa kudai inahujumiwa na baadhi ya madereva kwa kisingizio cha kucheleweshewa mishahara yao.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Oktoba 10, 2018 msemaji wa Udart, Deus Bugaywa amesema leo mabasi hayo yamechelewa kuanza kazi kwa sababu kuna gari lilienda kupaki kwenye geti la nyuma ambalo mabasi yanatokea na mhusika kutokomea kusikojulikana.

"Kwa kawaida mabasi huwa yanaanza kutoka saa 9 usiku lakini leo yamechelewa kwa sababu kuna gari lilikwenda kupaki kwenye geti. Tulifanya jitihada za kulitoa na mabasi yakaanza kutoka saa 11, alfajiri," amesema.

Bugaywa amesema wanafanya uchunguzi kubaini wanaohusika na hujuma hizo na kwamba watashirikisha vyombo vya dola katika mchakato huo.

Amesema suala hilo limeharibu mtiririko wa magari leo na kusababisha adha kwa watumiaji wa usafiri huo hasa wakati wa asubuhi.

"Tunaomba radhi kwa wananchi wote ambao leo wamepata shida vituoni. Hii imetokana na hujuma tunayofanyiwa na baadhi ya watu wasiotambua umuhimu wa usafiri huu," amesema.

Msemaji huyo ameongeza kwamba miezi mitatu iliyopita walifukuza madereva 15 waliobainika kuihujumu kampuni hiyo kwa namna mbalimbali.

Amesema hawatasita kuwachukulia hatua pia watakaobainika kwenye hujuma hiyo.

"Si mara ya kwanza suala hili kutokea, kuna kipindi ilikuwa lazima basi liharibike njiani linapofika Kimara, ili mradi tu kuharibu flow ya mabasi," amesema.