Home | Terms & Conditions | Help

November 30, 2024, 8:32 am

NEWS: CHINA YAIPA MSAADA TANZANIA WA TSH. BIL 146 UJENZI WA RELI YA SGR

Serikali ya Tanzania imepokea msaada kutoka serekali ya Jamhuri ya watu wa China ya Shilingi Bilioni 146.47. makubaliano hayo yamesainiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dotto James na Balozi wa China nchini Wang Ke Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kwa niaba ya serekali ya Tanzania Leo Mei 19, 2018 baada ya kusaini mkataba huo Katibu Mkuu alisema kuwa fedha hizo ni msaada na siyo mkopo na zitatumika katika miradi miwili ya miundombinu. Mradi wa kwanza ni ujenzi wa Chuo Kikuu cha Usafirishaji cha Taifa (NIT) ambacho kitajengwa Mabibo Jijini Dar es Salaam kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 62 sawa na takriban Shilingi bilioni 138.3. Mradi wa pili ni kwa ajili ya kusaidia upembuzi yakinifu na upembuzi sanifu wa mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (SGR), ambapo kiasi cha Sh. bilioni 3.2 kimetengwa kwa ajili hiyo. Bw. Doto James alisema kwa sasa mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha Kimataifa umeanza kwa awamu mbili ambazo moja ni kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro, na kuanzia Morogoro hadi Makutopora Dodoma,

upembuzi yakinifu utakaofanywa na Serikali ya China ni kwa maeneo mengine ya ujenzi wa Reli hiyo kuanzia Dodoma, Tabora hadi Mwanza na Kuanzia Kaliua hadi Kigoma. "China imetusaidia miradi mingi ikiwemo mradi wa maji Chalinze, Ujenzi wa uwanja wa Michezo wa Taifa, Mradi wa teknolojia za Kilimo mkoani Morogoro, Kituo cha upasuaji wa moyo na mafunzo, Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Nyerere pamoja na misaada ya dawa na vifaa tiba" alieleza Bw. James Kwa upande wake Balozi wa China hapa nchini, Wang Ke, Alisema kuwa China inategemea kuona kuwa msaada huo utasaidia kuimarisha maendeleo na kuisaidia Tanzania kupata maendeleo haraka. Aidha alisema China itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo ambayo itawasaidia Watanzania na kuendeleza urafiki uliopo kati ya nchi hizi mbili.

Balozi Wang Ke, amesema Pia Serikali ya China na Tanzania zinaendelea majadiliano kuhusu ujenzi wa bandari ya Bagamoyo, na kuongeza kuwa majadiliano hayo yatakapokamilika nchi yake itasaidia ujenzi wa bandari hiyo. Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Usafirishaji Taifa (NIT) Prof. Zacharia Mganilwa ameishukuru Serikali ya China kwa msaada huo na kusema kuwa msaada huo utaisaidia chuo hicho kuweza kutoa wataalamu wa kutosha kuweza kushiriki katika ujenzi wa miundombinu ikiwemo sekta ya anga. Amebainisha kuwa Chuo hicho Kikuu kitatoa mafunzo kwenye fani muhimu na zinazohitajika ikiwemo ufundi wa reli, masuala ya anga na sekta nyingine mtambuka kwa kutoa wataalamu waliobobea watakao changia kufanikisha azma ya Serikali ya uchumi wa viwanda.