Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 5:48 am

NEWS: CHADEMA YAKANUSHA KUHISIKA NA MATUKIO YA UTEKAJI

Dar es Salaam: Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimekanusha kuwa hakijihusishi na matukio yeyote ya utekaji na utesaji kwa maelezo kuwa tuhuma hizo ni propaganda za watu fulani.

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Oktoba 18, 2018 na naibu katibu mkuu wa chama hicho (Bara), John Mnyika wakati akijibu swali katika mkutano na waandishi wa habari.

Mkutano huo ulifanyika kwa ajili ya kueleza maazimio ya kikao cha kamati kuu ya Chadema kilichokutana jana kuwahoji na kuwajadili wabunge wake, Anthony Komu (Moshi VIjijini) na Saed Kubenea wa Ubungo.

Katika mkutano huo waandishi walitaka kujua kama kilichofanywa na wabunge hao kinaweza kuhusishwa na matukio ya utekaji yanayoendelea nchini.

Akijibu swali hilo, Mnyika amesema, “Chadema haina mikakati ya utekaji au utesaji au mikakati mingine haramu kwa hiyo hizo zinazosemwa ni propaganda. Kama ingekuwa kweli nguvu yote ya dola ingeelekezwa kwetu.”

Wabunge hao walihojiwa kuhusu sauti zilizosambaa katika mitandao ya kijamii wakisikika wakipanga mpango hasi dhidi ya Meya wa Ubungo, Boniface Jacob.

“Tulitoa agizo jana (kwa Kubenea na Komu) waandike barua na leo asubuhi wameziwasilisha. Kinachoendelea sasa hawa wabunge wapo chini ya uangalizi ni matarajio yetu watabadilika na hili ni funzo kwa wanachama wote na viongozi wazingatie katiba, kanuni na maadili ya chama,” amesema.

Amesema katika kipindi hiki ambacho hatushiriki kwenye chaguzi ndogo nguvu zetu zote tunazielekeza kwenye ujenzi wa chama.

“Jambo hili la ujenzi wa chama ni muhimu zaidi katika safari ya kuiondoa CCM madarakani. Tunakwenda kujichimbia mikoani kwa kazi ya ujenzi wa chama na tutafanya mikutano ya ndani kuhakikisha tunafanya mabadiliko makubwa zaidi.”

Kuhusu tuhuma za kumdhuru Meya Jacob ambaye ni diwani wa ubunge, Komu amesema, “Kumdhuru Boni tulishaeleza katika kamati kuu na imeonekana hakuna suala kubwa.”

“Kilichopelekea kuonekana tuna mpango wa kumdhuru ni kwa sababu hii ‘clip’ ilitoka kwa bahati mbaya na kila mtu akatafsiri kwa maana yake kwa sababu sisi tulisema kumtoa kwa hiyo tafsiri ya kudhuru imetolewa na watu,” amesema

Akijibu swali lililotaka kujua kama siku wanazungumza walikuwa wamelewa au la, Komu amesema, “Hatukuwa tumelewa, tulikuwa wazima ndani ya gari na mazungumzo yalianzia mbali hadi kufikia huko.”

“Hakuna hujuma yoyote ambayo tulikuwa tumeipanga, tulikuwa na mazungumzo mengine yakaingilia kati,”