Hukumu hiyo imetolewa leo na Jaji Sam Rumanyika aliyekuwa anaendesha kesi hiyo, na kusema kwamba mshtakiwa amekutwa na hatia ya kuua bila kukusudia kutokana na ushahidi wa mazingira, hivyo atatumikia kifungo cha miaka miwili jela.
"Ushahidi wa mazingira unaweza kutumika kama msingi pekee wa kumtia hatiani mshtakiwa tena mshtakiwa pekee, sasa ninapokwenda kuangalia maelezo ya mshtakiwa kama yanakidhi vigezo nilivyosema awali, kwa mujibu wa mshtakiwa alisema alianza kupigwa na marehemu, marehemu alilewa lakini mshtakiwa alitakiwa kutoa maelezo yanayo jitosheleza, kwa hili mshtakiwa alijikanganya", amesema Jaji Rumanyika.
Jaji Rumanyika ameendelea kwa kusema kwamba.."mshtakiwa katika maelezo yake hakueleza kuwa marehemu alianguka au laah wakati anamkimbiza, maelezo ya Dkt. Josephine siyo maelezo ya cheti cha hospitali, hayakuwa na hadhi ya hospitali".
"Inakinzana na hekima ya kawaida kwamba hata pale marehemu alipoendelea kumpiga na kumshambulia na akaenda kiwango cha kumtishia kumuua, mstakiwa hakuthubutu hata kumpiga, ina maana alifanya kama maneno ya biblia yanavyosema mtu akikupiga shavu la kushoto mgeuzie na la kulia lakini hili mshtakiwa hakulisema.", amesema Jaji Rumanyika.
"Na wakati huo mshtakiwa alikuwa na miaka 17, leo ana miaka 22, alikuwa mtoto hivyo asingetambua kuwa kinachofanyika ni kibaya au kizuri, lakini huyu mtoto sio mshtakiwa aliyelengwa nasheria ya watoto, kama mtoto wa umri huu na anaweza kafanya ya watu wazima, mahakama hii haikubaliani bali mshtakiwa ni mkomavu, hakuna mashaka kuwa kifo cha marehemu kilitokana na ugomvi", ameendelea kusema Jaji Rumanyika mahakamani hapo.
Baada ya hapo Jaji Rumanyika aliwapa nafasi upande wa mshtakiwa kujitetea ambapo wakili wake Peter Kibatala alimtetea mshakiwa kwa kusema kuwa mshtakiwa anategemewa na familia yake akiwemo mama yake na mama yake mdogo.
Baada ya hapo Jaji Rumanyika alitoa hukumu yake na kumuamuru mshtakiwa kwenda jela kwa miaka miwili.
Elizabeth Michael (Lulu) anahukumiwa kwa kumuaa aliyekuwa mpenzi wake Steven Charles Kanumba ambaye pia ni muigizaji mwenzake, mnamo April 7, 2012.