Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 3:51 am

NEWS : AMISOM KUONDOKA NA ASKARI 1000 NCHINI SOMALIA

AMISOM kuondoa askari 1,000 nchini Somalia licha ya kuendelea kukosekana uthabiti nchini humo

AMISOM kuondoa askari 1,000 nchini Somalia licha ya kuendelea kukosekana uthabiti nchini humo

Ujumbe wa Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) umetangaza kuwa utaondoa askari 1,000 kutoka Somalia kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika nchini Somalia, Francisco Madeira amesema kuwa AMISOM imeanza kupunguza idadi ya askari wake nchini humo na kwamba kufikia tarehe 31 Disemba mwaka huu wa 2017,askari 1000 wa kikosi hicho watakuwa wameondoka katika ardhi ya Somalia.

Madeira amesisitiza umuhimu wa kuwepo umoja kati ya raia na jeshi nchini Somalia dhidi ya ugaidi na kusema jeshi pekee haliwezi kuwashinda magaidi bila ya msaada wa raia. Amewataka Wasomali wote kushirikiana kwa ajili ya kuwafukuzia mbali magaidi wa kundi la kigaidi la al Shabab.

Aidha amesema ifikapo mwisho wa mwaka 2020, askari wote wa AMISOM watakuwa wamekamilisha majukumu yao ya kulinda amani na kutoa mafunzo kwa polisi na jeshi la Somalia na hivyo katika kipindi hicho wataondoka nchini humo.

Kikosi cha majeshi ya Umoja wa Afrika, AMISOM ambacho kiliundwa kupitia azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kimekuwa kikiisaidia serikali ya Somalia kupambana na magaidi wa kundi la al Shabab tangu mwaka 2007.

Kikosi hicho kinaundwa na askari elfu 22 kutoka nchi za Uganda, Kenya, Djibouti, Burundi na Ethiopia.

Magaidi wa al Shabab wamezidisha mashambulizi ya kujilipua kwa mabomu katika wiki za hivi karibuni hususan katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu

AMISOM imetangaza kuanza kuondoa askari wake Somalia katika hali ambayo magaidi hivi karibuni walitekeleza hujuma katika mji mkuu Mogadishu mnamo Oktoba 14 na kuua watu zaidi ya 350 katika shambulizi lililotajwa kuwa baya zaidi katika historia ya Somalia.

Baada ya hapo pia watu kadhaa wameuawa katika mashambnulizi ya kigaidi mjini Mogadishu ambapo kundi la kigaidi la Al Shabab limedai kuhusika.

Somalia ni nchi iliyo katika Pembe ya Afrika na inahesabiwa kuwa kati ya nchi masikini zaidi isiyo na uthabiti duniani. Aidha nchi hiyo mara kwa mara hukumbwa na ukame huku ikiendelea kusakamwa na jinamizi la magaidi wakufurishaji wa al-Shabab na hivyo kufanya maisha yawe magumu mno kwa wananchi.

Hali baada ya hujuma ya kigaidi mjini Mogadishu

Kwa miongo mitatu sasa Somalia imekuwa medani ya vita na machafuko na ndio jamii ya kimataifa ikaamua kuunga mkono serikali kuu yenye makao yake Mogadishu ili kwa njia hiyo kujaribu kurejesha uthabiti nchini humo.

Kundi la kigaidi la Al Shabab linalofungamana na mtandao wa Al-Qaeda linataka kuiangusha serikali ya Somalia huku kukiwa na ripoti kuwa magaidi wa ISIS au Daesh sasa wameanza kuenea nchini humo.

Pamoja na kuwepo jitihada za askari wa kulinda amani wa AMISOM lakini magaidi wa al Shabab wangali wanashikilia maeneo mengi ya Somalia jambo llinalowawezesha kutega mabomu katika maeneo mbali mbali ya nchi hiyo.