Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 9:47 pm

NEWS: ABIRIA WALIPONZA BASI LA IMMO EXPRESS NA SPIDER, YAKUMBANA NA RUNGU LA MANISPAA.

DODOMA: Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma imeendelea kuwakumbusha wakazi wa Manispaa kuendelea kuzingatia suala la usafi wa Mazingira na kutotupa taka ovyo katika lolote ndani Manispaa hiyo kwani atakayefaya hivyo atapambana na mkono wa sheria ikiwemo kulipa faini inayoanzia shilingi 50,000 hadi 300,000 au kutumikia kifungo cha miezi sita jela.

Rai hiyo pia inawahusu wasafiri wote wanaoingia Mjini Dodoma au kupitia wakielekea mikoa mingine kwamba wajiepusha kutupa uchafu ovyo nje ya vyombo vyao vya usafiri ikiwemo mabaki ya vyakula kwani wakibainika watachuliwa hatua za kisheria kama wachafuzi wengine.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Idara ya Mazingira na Usafishaji wa Halmashauri hiyo Dickson Kimaro jana wakati alipowaongoza askari Jamii wa Manispaa hiyo kukamata mabasi ya Kampuni ya Immo Express na Spider baada ya baadhi ya abiria waliokuwa wakisafiri na mabasi hayo kudaiwa kutupa uchafu katika eneo la Nala barabara kuu ya Dodoma-Singida, ikiwemo mifuko ya plastiki iliyokuwa na mabaki ya vyakula.

Kufuatia tukio hilo, mabasi hayo yalitozwa faini ya Shilingi 50,000 kwa kila kampuni na baada ya kulipa yaliachiwa na kuendelea na safari.

Manispaa ya Dodoma imejipanga kikamilifu katika kuhakikisha Mji Mkuu wa Nchi unakuwa safi muda wote, ambapo hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dokta Binilith Mahenge alitangaza Kampeni ya Usafi wa Mazingira mjini humo ambapo sasa usafi utafanyika Jumamosi ya kila wiki.

Katika utaratibu huo, Wananchi wote wanatakiwa kufanya usafi katika maeneo yao ya makazi, maeneo ya biashara, na maeneo ya wazi.