Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 11:47 am

NEWS: 13 WAJERUHIWA, 2,375 HAWANA MAKAZI.


Mwanza. Watu 13 wamejeruhiwa na nyumba 479 zimeharibiwa na mvua ya upepo wilayani Kwimba mkoani Mwanza.

Miongoni mwa majengo yaliyoharibika kutokana na mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia jana Jumanne na leo Jumatano ni madarasa mawili ya Shule ya Msingi Mangulumwa na maabara ya Shule ya Sekondari Igongwa.

Kutokana na mvua hiyo, wakazi 2,375 hawana makazi.

Kati ya waliojeruhiwa leo Jumatano ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Mangulumwa walioangukiwa na paa la darasa walimokuwa wamejihifadhi wakati mvua ikinyesha.

Akizungumza na Mwananchi baada ya kutembelea maeneo yaliyoathiriwa, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Mtemi Msafiri amesema kati ya majeruhi hao, mmoja ni Shida Masuka (10), mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Mangulumwa.

Amesema mwanafunzi huyo amejeruhiwa maeneo mbalimbali ya mwili na anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza.

Majeruhi wengine waliolazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba wametajwa kuwa ni Shani Shija (11), Mashara Luhemea (11) na Angelina Pastori (11), wanafunzi wa Shule ya Msingi Mangulumwa na mkazi wa kijiji hicho, Mpemba Lufuga (72).