Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 2:57 pm

NEES: UCHAGUZI CONGO WASOGEZWA MBELE MPAKA MARCH

Tume ya Uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, imetangaza kuahirisha Uchaguzi Mkuu wa siku ya Jumapili, katika majimbo ya Beni na Butembo, Mashariki mwa nchi hiyo.

Taarifa kutoka kwa Tume hiyo, zimesema, sababu ya uchaguzi huo kuahirishwa hadi mwezi Machi mwaka 2019, ni kwa sababu ya changamoto za kiusalama katika maeneo hayo ambayo yameendelea kushuhudia mashambulizi ya makundi ya waasi.

Kabla ya kutolewa kwa tangazo hili, Tume ya Uchaguzi ilionesha wasiwasi wake kuhusu usalama wa wafanyikazi na vifaa vya kupigia kura katika Wilaya ya Beni, ambayo wakaazi wameendelea kusumbuliwa na waasi wa ADF NALU.

Wiki moja iliyopita, ghala la kuhifadhi vifaa vya kupigia kura, pia viliteketea moto katika wilaya ya Beni.

Aidha, mwishoni mwa wiki iliyopita, watu watano waliuawa baada ya kushambuliwa na waasi wa ADF, na kuzua wasiwasi wa iwapo Uchaguzi huo utafanyika katika eneo hilo ambalo pia pia linasumbuliwa na maambukizi ya ugonjwa hatari wa Ebola.

Eneo lingine ambalo Jumapili uchaguzi hautafanyika kwa sababu za kiusalama ni Yumbi, linalopatikana katika mkoa wa Mai-Ndombe Kusini Magharibi mwa nchi hiyo.

Tayari Uchaguzi nchini DRC umeahirishwa mara tatu tangu 2016, katika taifa hilo ambalo linaongozwa na rais Joseph Kabila ambaye muda wake unakaribia kufika mwisho baada ya kuongoza kwa miaka 17.