Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 11:32 am

MAKALA:"RAIS WA CCM J.P MAGUFULI ANACHUKIA DEMOKRASIA" ZITTO KABWE

Inaandikwa na Mh. Zitto Zubiri Kabwe

Dar es salaam: Mwezi Agosti mwaka huu, 2017, niliandika makala fupi kwenye ukurasa wangu wa Facebook kwamba sisi tulio hai tunawajibu wa kulinda kazi za Waasisi wa Demokrasia ya Vyama vingi nchini Tanzania. Nilionya kuhusu mpango wa Serikali ya CCM ya Awamu ya Tano kutunga sheria itakayoweka mazingira magumu Kwa vyama vya upinzani kufanya shughuli zake. Muswada wa sheria hiyo Sasa upo tayari na umesambazwa Kwa Vyama. Muswada huo ni hukumu ya kunyongwa mpaka kufa Kwa vyama vya Upinzani nchini Tanzania. Ni vifungu 71 vya Hukumu ya Kifo.

Rais wa CCM John Pombe Magufuli anachukia demokrasia. Anaona vyama vya siasa ni bugudha. Anatamani hata hiyo CCM isiwepo atawale Kama Mfalme ( absolute monarchy). Anakosea Sana. Kuna watu walipoteza maisha Yao kwa ajili ya kupigania uwepo wa Demokrasia nchini kwetu. Haikuja tu. Haikushuka kutoka mbinguni. Ilipiganiwa kwa jasho na damu. Watanzania wa Sasa hawatakubali Nchi kurudi kwenye utawala wa Chama kimoja kamwe. Demokrasia ya Nchi yetu sio hisani ya CCM wala Magufuli bali ni matokeo ya mapambano ya Watanzania.

Sheria mpya ya vyama vya siasa inataka kuzuia kisheria mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa isipokuwa mwaka wa uchaguzi tu. Kama CCM inaona inafanya kazi vizuri ya kuleta maendeleo kwanini inaogopa mikutano? Kifungu cha 45 cha muswada huo kinasema:

45- (1) Every party which has been provisionally or fully registered shall be entitled:-

a)to hold and address public meetings in any area in the United Republic after giving notification to the police officer in-charge of the area concerned for purposes of publicizing itself and soliciting for membership;

(b) to the protection and assistance of the Government security group for the purposes of facilitating peaceful and orderly meetings

(c) to the provision by the State, of fair opportunity to present the political party’s programmes to the public by ensuring equitable access to the State owned media.

Halafu kinaendelea

(2) Notwithstanding the provisions of subsection (1) and any other written law, a political party shall not hold public meeting or rally or procession before or after election period unless the public meeting is hosted by elected member of parliament or house of representative in his/her constituency or elected local councilor in his/her ward or parliamentarian/house of representative or councilors women special seats in their jurisdiction and other elected members in their electoral jurisdiction.

Yaani 45(1) inatoa ruhusa Kwa vyama kufanya mikutano halafu 45(2) inasema watakaofanya mikutano ni wabunge na madiwani tu kwenye maeneo yao.

Tutaipinga sheria Hii dhalimu ndani na Nje ya Bunge. Tutalinda Mfumo wa Vyama vingi nchini kwetu kwa gharama yeyote ile kwani uwepo wa vyama ni haki ya kikatiba na haki hiyo haiwezi kunyanganywa na mtu mmoja eti Kwa sababu tu anaishi Ikulu. Watanzania tujiandae Kwa harakati za kuilinda na kuitetea Katiba yetu. Kazi kubwa kuliko zote za Jeshi la Wananchi ( JWTZ ) ni KULINDA KATIBA. Wananchi Ndio jeshi la mstari wa mbele la ulinzi wa Katiba. Tusimame kukataa kurudishwa kwenye Chama kimoja. Umoja wa Ulinzi wa Demokrasia ( Democratic Front ) Ni muhimu zaidi Hivi sasa kuliko wakati wowote katika miaka 25 ya uwepo wa demokrasia yetu.

Tukatae Hukumu ya Kifo cha Demokrasia inayokuja Kwa mtindo wa vifungu 71 vya Sheria mpya ya vyama vya siasa ( The Political Parties Act 2017 ).

Hii hapa chini ni makala niliyoandika Mwezi Agosti.

Tulinde kazi ya Waasisi wa Mageuzi nchini

Zitto Kabwe
Agosti 30, 2017

ACT Wazalendo tumepokea barua ya kututaka kutoa maoni ya kuandikwa upya Kwa sheria ya vyama vya siasa. Barua ni ya jumla mno na tumepewa wiki mbili tu kutoa maoni bila mwongozo wowote.

Kufuatia uzoefu wa sheria ya Habari iliyopitishwa Kwa nguvu na kuanza kuleta taharuki Kwa Uhuru wa Habari nchini na ugandamizwaji wa Uhuru wa kidemokrasia unaoendelea Sasa dhidi ya vyama vya siasa, ninaona dhahiri kuwa sheria hii mpya ya vyama vya siasa inakwenda kunyonga vyama.
Nimesoma kwenye Gazeti la The Citizen kuhusu mabadiliko yanayopendekezwa. Miongoni mwayo ni kuweka ukomo wa mihula Kwa Viongozi wa vyama, suala la polisi kuzuia mikutano ya vyama vya Siasa, mamlaka ya Msajili kufuta Vyama Mwaka wa uchaguzi na mamlaka ya Msajili kutaka Taarifa yeyote kutoka kwenye Vyama. Mapendekezo haya hayahitaji kuandikwa upya kwa sheria kwani ni madogo Sana na mengi hayakubaliki kwani yanaweza kuamuliwa na vyama vyenyewe Kwa mujibu wa Katiba zao.

Ninatoa wito kuwa Baraza la Vyama vya siasa liitwe mara moja na kujadili ni mabadiliko gani yanatakiwa. Nawasihi Viongozi wote wa vyama kuungana kulinda mfumo wetu wa demokrasia ya vyama vingi.

Waasisi wa mageuzi wa Mwaka 1990-1992 wakina Mabere Nyaucho Marando, Mashaka Nindi Chimoto, Prince Mahinja Bagenda, Edwin Mtei, Bob Makani, Freeman Mbowe, Ringo Tenga, Masumbuko Lamwai, Daniel Nsanzugwanko, Joseph Selasini, James Mbatia, Antony Kalisti Komu, Jafari Kasisiko, Msafiri Mtemelwa, James Mapalala, Maalim Seif Sharif Hamad, Shaaban Mloo, Hamad Rashid Mohammed na wengine wengi walitoa jasho na damu kufikia hapa tulipo kwenye sheria Hii. Haikuwa kazi rahisi. Mfumo wa Vyama vingi ulipiganiwa Kwa nguvu kubwa na mashujaa wa Mageuzi, sio wote wamenufaika binafsi lakini nchi ilinufaika. Mfumo wa vyama vingi ulianza kushika mizizi na kuwa utamaduni mzuri Kwa wananchi wetu. Sheria mpya inakwenda kufifisha juhudi za ukombozi za waasisi wa mageuzi nchini kwetu. Tusikubali.

Sisi tuliopo Sasa tuna wajibu wa kulinda mfumo wa demokrasia ya vyama vingi Kwa gharama yeyote ile. Tusiruhusu mtu yeyote aturudishe nyuma kwenye utawala wa Imla.

( Mwisho wa Makala).

Zitto Kabwe

Ujiji, Kigoma
13/10/2017