Home | Terms & Conditions | Help

December 3, 2024, 8:57 pm

MAKALA: Mfaham Rais Dr. John Pombe Magufuli(Rais wa Jamhuri ya Muungano wa TANZANIA), kuanzia kuzaliwa kwake mpaka sasa.

Dar es salaam. Leo tuna kuwakilishia historia ya Raisi wa awamu ya tano wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dr John Magufuli, ambaye alichukuwa kijiti cha urais oktoba mwaka jana, leo hii katimiza mwaka mmoja toka ashike madaraka, kama Rais.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John P. Magufuli alizaliwa Oktoba 29, 1959 Wilayani Chato Mkoa wa Kagera ambayo hivi sasa ipo Mkoa wa Geita. Dkt. Magufuli amemuoa Mwalimu Janet na wamejaliwa kupata watoto.

Kazi yake

Mwaka 1982 hadi 1983 alikuwa Mwalimu Shule ya Sekondari Sengerema akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati na mnamo mwaka 1989 hadi 1995 alikuwa Mkemia wa Chama cha Ushirika cha Nyanza (Nyanza Cooperative Union Ltd) Mwanza.

Harakati zake za kisiasa zilianza mwaka 1995 alipogombea kiti cha ubunge katika jimbo la Chato na kuteuliwa kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Ujenzi. Mwaka 2000 Dkt. Magufuli aligombea na kushinda kwa mara ya pili na kuteuliwa kuwa Waziri wa Wizara ya Ujenzi.

Aidha, katika chaguzi za mwaka 2005 na 2010, aliendelea kuwania kiti cha ubunge katika jimbo la Chato na kushinda uchaguzi huo na kuteuliwa kuwa Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hadi mwaka 2008 alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambayo aliiongoza hadi mwaka 2010. Mwaka 2010 alipochaguliwa tena kuwa mbunge wa Chato aliteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi.

Elimu yake

Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alipata elimu ya msingi katika shule ya msingi Chato kuanzia mwaka 1967 hadi 1974. Pia alijiunga na elimu ya Sekondari katika shule ya Seminari Katoke-Biharamulo na Lake Sekondari-Mwanza kati ya mwaka 1975 hadi 1978. Aidha, mwaka 1979 hadi 1981 aliendelea na masomo yake ya kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Mkwawa Mkoani Iringa.

Dkt. Magufuli pia alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria akianzia Makutupora, Dodoma (Julai - Desemba 1983), kisha akaenda kambi ya Makuyuni, Arusha (Januari hadi Machi 1984) na akamalizia katika kambi ya Mpwapwa mkoani Dodoma (Machi – Juni 1984). Mwaka 1985 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akisomea Shahada ya Sayansi ya Elimu akibobea kwenye masomo ya Kemia na Hisabati na alihitimu mwaka 1988.

Kati ya mwaka 1991 na 1994 alijiunga na masomo ya Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Chuo Kikuu cha Salford nchini Uingereza na baadaye mwaka 2006-2009 alijiunga na masomo ya Shahada ya Uzamivu ya Kemia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kutokana na taaluma yake Dkt. Magufuli ameandika vitabu na machapisho mbalimbali.