Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 4:06 pm

MAHUSIANO: KWANINI WATU WENGI WANAANGUKA KATIKA ZINAA?.

Tuko katika kipindi ambacho pepo la zinaa linatenda kazi kwa kasi ya ajabu. Shetani amebuni mbinu nyingi za kuwafanya watu wazini na kuhalalisha uzinzi wao.


Kumbuka shetani amemzidi mwanadamu kwa kiwango kikubwa. Tunamshinda pale tu tunapokuwa tumempokea Yesu na kutambua na kutumia mamlaka aliyotupa. Ufunuo wa Yohana 12:11 “Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.” Tunashinda kwa DAMU YA YESU KRISTO (imani katika Yesu), USHUHUDA WA NENO (kuwaambia wengine kuhusu Mungu) na KUTOPENDA MAISHA HATA KUFA (kujitoa kwa Mungu kwa gharama yoyote hata ikibidi kufa).
Ni ukweli usiopingika kwamba mwanadamu bila Yesu hawezi kumfanya chochote shetani:

1. Shetani anamjua Mungu kuliko mwanadamu maana alikuwa mbinguni kabla ya uasi. Anajua uzuri wa mbinguni ndiyo maana hataki kuona mtu anaingia mbinguni.

2. Shetani anajua Biblia kuliko mwanadamu yeyote maana alikuwepo mbinguni na wakati manabii na mitume wanaandika alikuwepo.

3. Shetani anamjua mwanadamu na udhaifu wake kuliko mwanadamu yeyote maana tangu mwanadamu anaumbwa alikuwepo na amemsoma kwa miaka mingi.
Hivyo hatuwezi kumshinda kwa kwenda kichwa kichwa bali kwa kanuni tulizopewa na Mungu. Ndiyo sababu tukaambiwa tuzijue fikra zake. 2 Wakorintho 2:11 “Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake.” Lakini pia shetani amejipanga kwa ngazi za utawala – FALME, MAMLAKA, WAKUU WA GIZA na MAPEPO. Waefeso 6:12 “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.” Lazima tujue tunapambana na ngazi ipi ya utawala wake na kwa silaha gani.
BWANA YESU ANAZUNGUMZIAJE UZINZI KATIKA AGANO JIPYA?
Mt 5:27-30 “Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini; lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake. Jicho lako la kuume likikukosesha, ling’oe ulitupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum. Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum.”
Katika Mathayo 5 Bwana alikuwa anatafsiri dhambi mbalimbali na matarajio kwa mujibu wa Agano Jipya. Kimsingi anasema KAMA MLIKUWA MNAHUKUMU UZINZI KWA KUMFUMANIA MTU AKIZINI, MIMI NAWAAMBIA KILA MTU ANAYETAMANI KWA MACHO TU AMESHAZINI NA ANASTAHILI JEHANAMU YA MOTO.
Kama tutashinda UZINZI WA MACHO kwa vyovyote vile hatutaweza kutekeleza UZINZI WA MWILI kwa sababu tunapotamani kwa macho ndipo tunaanza mipango kichwani na kisha kuchukua hatua za kutekeleza uzinzi kimwili. Mara nyingi watu tunaoshangaa kwamba wameanguka katika dhambi ya uzinzi walianguka siku nyingi tunachokiona ni USHAHIDI TU wa dhambi yao.
Bwana Yesu anasema maneno mazito sana anaposema ‘JICHO LAKO LA KUUME LIKIKUKOSESHA, LING’OE ULITUPE MBALI NAWE; KWA MAANA YAKUFAA KIUNGO CHAKO KIMOJA KIPOTEE WALA MWILI WAKO MZIMA USITUPWE KATIKA JEHANUM.’ Afadhali uende mbinguni una chongo kuliko kuwa na macho mazima na kuishia Jehanamu.
KWA NINI HATA WATU WA MUNGU WANAANGUKA KATIKA ZINAA?
1. Kutazama visivyofaa.
Zaburi 119:37 “Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa, Unihuishe katika njia yako.” Unapotazama visivyofaa lazima mwili wako utanajisika. Lazima kuepuka kutazama picha zinazokusisimua mwili kupitia TV (tamthilia, maigizo, miziki nk) na Internet (picha za ngono nk). Tufanye maamuzi kama alivyofanya Ayubu. Ayubu 31:1 “Nilifanya agano na macho yangu; Basi nawezaje kumwangalia msichana?” Hapa hazungumzii kumtazama kwa kawaida. Biblia ya kingereza imeeleza wazi zaidi kwa kusema “Nilifanya agano na macho yangu nisimtazame msichana kwa tamaa.” (I made a covenant with my eyes not to look lustfully at a young woman). Mwili utatupeleka pabaya kama hatutaweza kuupangia. 1 Wakorintho 9:27 “bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.” Mtume Paulo aliamua kuutesa na kuutumikisha mwili asije akahubiri na mwishowe akakataliwa (disqualified).
Shetani amejipanga sana. Video chafu ulizokimbia nyumbani unakutana nazo kwenye basi ukisafiri. Kuna picha za aibu kwenye mabasi mpaka najiuliza hivi mamlaka zinazohusika kwa nini zimefumba macho. Hata hivyo huwezi kujitetea kwamba uliwakwa tamaa ukiwa kwenye basi. Njia ninayotumia mimi ni kuhakikisha nina kitabu nasoma au tablet ili nisishawishike kuangalia video chafu. Shetani anapenda kumtumia mtu ambaye hana cha kufanya (An idle mind is devil’s workshop). Katika tamthilia nyingi ambazo wengi wanadhani zina mafundisho utagundua kwamba kama yapo ni asilimia 5 hadi 10 tu. Sehemu kubwa ni ZINAA, UCHAWI na MAUAJI. Mit 5:25 “Usiutamani uzuri wake moyoni mwako; Wala usikubali akunase kwa kope za macho yake.”
2. Kutokuwa na mipaka katika mahusiano
2 Kor 6:14,17 “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha.” Kwa muda mrefu andiko hili limetumiwa kimapokeo kumaanisha kwamba ukiokoka unatakiwa utoke dhehebu fulani uingie dhehebu jingine. Maana ya andiko hili ni pana sana. Kwanza lazima tujue kwamba mtu anaweza kuwa mshirika/msharika wa dhehebu lenye misingi mizuri na wakati huohuo awe haamini. Kama hawangekuwepo watu wasioamini katika makanisa hapangetokea watu kuanguka dhambini. Kwa hiyo hata ndani ya kanisa hilohilo kuna watu tunatakiwa KUTOKA KATI YAO NA KUTENGWA NAO.
Kwa vile hakuna mipaka katika mahusiano kwa kisingizio kwamba ni mpendwa wa kanisani, wengi wamejikuta wakianguka. Lazima tuwe na mipaka katika mahusiano na watu wa jinsi tofauti ambao sio mume na mke. Tuepuke kukutana mazingira hatarishi, kuzoeana kulikopitiliza na kuwa na ukaribu usio na sababu. Tuwe na ujasiri wa kuonyana. Mit 6:27-29 “Je! Mtu aweza kuua moto kifuani pake, Na nguo zake zisiteketezwe?Je! Mtu aweza kukanyaga makaa ya moto, Na nyayo zake zisiungue? Ndivyo alivyo aingiaye kwa mke wa jirani yake; Kila mtu amgusaye huyo atakuwa na hatia.” Je unaweza kuwa karibu sana na mtu wa jinsi nyingine ambaye si ndugu wa karibu mwili wako usisisimke? Tukitaka kuwa salama lazima iwepo nafasi ya kutosha katika mahusiano ya watu wa jinsi tofauti. Dhambi ya zinaa inatendwa katika mwili hivyo ukiwepo umbali kimwili haiwezi kutendeka. Ziko dhambi tunazishinda kwa kukemea lakini zinaa tunaishinda kwa KUKIMBIA. 1 Wakorintho 6:18 “Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.”
3. Kupenda faragha na watu wa jinsi tofauti mkiwa wawili tu
Mwa 39:11,12 “Ikawa, siku moja, akaingia nyumbani atende kazi yake, wala hapakuwa na mtu katika watu wa nyumbani humo ndani; huyo mwanamke akamshika nguo zake, akisema, Lala nami. Yusufu akaiacha nguo yake mkononi mwake, akakimbia, akatoka nje.” Najua sio wakati wote inawezekana kukwepa mazingira ya faragha kulingana na aina ya kazi anayofanya mtu kama ilivyokuwa kwa Yusufu. Lakini wengi wetu tunaaminiana sana mpaka tunaamua kuomba chumbani wawili tu huku milango imefungwa. Mnapozoea kuwa karibu mnaanza kutengeneza ukaribu (bond) maana maumbile tofauti yanaleta mvuto (opposites attract) hivyo mtaanza taratibu kuhama katika agenda yenu na kuanza kuwa marafiki na mwisho mtakuwa wapenzi. Ukaribu unaweza kumfanya mtu ambaye awali ulikuwa unamuona hakufai na hana sura nzuri akianza kukuvutia. Ili kuepuka mitihani hii ni vizuri kuwa watatu au watano lakini katika mazingira ya wazi. Sio tu kwamba itakusaidia uepuke majaribu lakini pia itakusaidia kulinda ushuhuda wako.
Lakini kuna wakati inabidi mtumishi aongee na mtu kibinafsi. Hata hivyo sio vizuri kuzoea kukutana mara kwa mara. Mfundishe kujisimamia na kuisimamia imani yake. Mtumishi sio Mungu wa kumuona kila wakati.
4. Kujiamini kupita kiasi
1 Kor 8:1b “Ujuzi huleta majivuno, bali upendo hujenga.” Ukiwa unajua mambo mengi ni rahisi kuwa na majivuno au kiburi. Na kiburi ndicho kinatangulia kuanguka. Mithali 16:18 “Kiburi hutangulia uangamivu; Na roho yenye kutakabari hutangulia maanguko.” Watu wengi wanaofanya huduma za ushauri nasaha na maombezi wanajiamini kupita kiasi hivyo hawachukui tahadhari katika huduma zao. Hata kama wewe hutajaribiwa moja kwa moja, unayemuombea anaweza kujaribiwa na kukutamani au anaweza kuongozwa na pepo la tamaa alilo nalo kukutamanisha. Kumbuka nimesema awali kwamba kuanguka sio kuzini kimwili bali ni kutamani kwa macho. Shetani anaweza kukuua kiroho kupitia tamaa ya macho.
Pale inapowezekana ni vizuri kufanya huduma katika mazingira ya wazi ambapo walio upande fulani wanawaona au wanaweza kufika mlipo bila kikwazo. Kama ni maombezi nyeti ni vizuri wawepo wasaidizi wengine. Kama anayeombewa ni mwanamke ni vizuri wawepo watu wa jinsi yake ili kusaidia kumshika au kumhudumia vizuri inapobidi (kwa wenye mapepo). Baadhi ya wenye pepo wakishikwa na watu wa jinsi tofauti pepo linapata nguvu ya kuleta ushawishi.
5. Mashambulizi ya shetani
Yuda 1:8 “Kadhalika na hawa, katika kuota kwao, huutia mwili uchafu, hukataa kutawaliwa, na kuyatukana matukufu.” Shetani anaweza kutuma pepo mbwa na kumvamia mtu. Kama mtu ametumiwa pepo hili na likamvaa hataweza kujizuia kumtamani mtu fulani. Atajikuta anamtamani mtu fulani mpaka anajisikia kuchanganyikiwa akili. Kumbuka Mungu wetu haleti roho ya kuchanganyikiwa (spirit of confusion). 1 Wakorintho 14:33 “Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amani; vile vile kama ilivyo katika makanisa yote ya watakatifu.” Lakini pia shetani anaweza kutuma pepo la mume/mke wa kiroho (spiritual husband/wife) na kumfanya mtu azini katika ndoto. Mwingine akiamka anajiona kabisa kwamba alifanya uzinzi dhahiri. Mapepo haya yanakuwa yamemuoa mhusika hivyo yatasababisha kama ameoa au kuolewa, asimpende mwenzi wake, asizae au afilisike katika uchumi wake. Yanaweza pia kumuua mwenzi wake au kuua uwezo wake wa kiume kwa vile yana wivu sana. Kama bado hajaolewa anaweza kutochumbiwa (anavalishwa sura ya mvulana au bibi mzee ili wanaume wasimsogelee), kuchumbiwa na kuachwa (kila uchumba unavunjika), kuchukia wanaume bila sababu, kuzalishwa na kuachwa nk.
Mtu mwenye mapepo anahitaji kuombewa na watumishi wenye mamlaka ili awekwe huru. Hata hivyo ni lazima awe tayari (apende) kuwekwa huru na ajue hatua za kuchukua akiwekwa huru ili asije akarudi nyuma na kuteseka zaidi na kisha kumlaumu aliyemuombea.
Lakini pia kuna mitego mingi ambayo inaandaliwa na adui ambayo inahitaji uangalifu na neema ya Mungu. Dada fulani kahaba aliposhindwa kumshawishi kaka mmoja aliyeokoka, aliamua kubuni mbinu. Alimtuma dada fulani amshtukize usiku kwenda kumuombea mgonjwa. Alipoingia ndani yule dada akafunga mlango kwa nje. Yule kaka akamkuta huyo dada kahaba ndani amevua nguo na akamuambia ukikataa nitapiga kelele kwamba umekuja kunibaka usiku huu. Lilikuwa jaribu zito kwa mtu wa Mungu lakini Mungu ashukuriwe alimpa mlango wa kutokea. Kwa mpagani hii ingekuwa ni fursa na sio jaribu.
Wapo waliolishwa uchawi (limbwata) na kujikuta anazini na mtu ambaye hata kibinadamu hamfananii. Mtu huyo ndiye anazipangia pesa zake kwa vile lengo la mhusika ni kumfilisi. Uchawi unaofanyika kwa ngono ni maagano yenye nguvu sana ya kummaliza mtu. Zaburi 91:3 “Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo.” Zaburi 141:9 “Unilinde na mtego walionitegea, Na matanzi yao watendao maovu.”
6. Kutoheshimu ndoa
Waebrania 13:4 “Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.” Kuna watu wanapenda kuwa karibu na watu wengine wa jinsi tofauti kuliko wenzi wao wa maisha. Ni vizuri kila mtu atambue na kutekeleza wajibu wake kwa mwenzi wake ili kuepuka mitihani inayoepukika. Ipo tamaa ya mwili ambayo inaweza kutimizwa kupitia ndoa na ipo tamaa mbaya ambayo hata kama mtu ameoa au kuolewa kama anayo itamsumbua tu. Tunatakiwa kuheshimu ndoa zetu na za watu wengine. 1 Kor 7:3,4 “Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake. Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe.” Wanandoa wanapozama kwenye kutafuta pesa na kusahau jukumu lao la msingi la ndoa, wanafungua mlango wa shetani kujipenyeza. Lazima kila mtu ajiulize na arejee nyuma na kujikumbusha kwamba ni nini hasa kilimsukuma kuoa au kuolewa. Kama tutarudi katika mpango wa asili wa Mungu kuhusu ndoa, shetani atakosa nafasi. Mwa 2:18,24 “Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye. Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.” Mungu alikusudia ndoa idhibiti upweke na kuwaunganisha wawili wawe mmoja. Leo hii tuna wanandoa wengi ambao ni wapweke (married singles).
7. Kuvaa mavazi na mapambo ya mapepo
Mit 7:10,11 “Na tazama, mwanamke akamkuta, Ana mavazi ya kikahaba, mwerevu wa moyo; Ana kelele, na ukaidi; Miguu yake haikai nyumbani mwake.” Mwa 35:3-5 “Tuondoke, tupande kwenda Betheli, nami nitamfanyia Mungu madhabahu huko; yeye aliyenisikia siku ya shida yangu, akawa pamoja nami katika njia yote niliyoiendea. Nao wakampa Yakobo miungu migeni yote iliyokuwa mikononi mwao, na pete zilizokuwa masikioni mwao, naye Yakobo akazificha chini ya mwaloni ulioko Shekemu. Wakashika njia, hofu ya Mungu ikaishika miji iliyowazunguka, wala hawakuwafuata wana wa Yakobo.” Mtu anapovaa mavazi ya kikahaba na mitindo ya kuzimu anafungua mlango wa kuvamiwa na mapepo maana anakosa UTISHO WA MUNGU. Ikiwa kwa kuvaa kwako unawafanya wanadamu barabarani wakutamani, je mapepo yaliyobuni mitindo ya mavazi uliyoyavaa? Mavazi halisi yana sifa zake. 1 Timotheo 2:9 “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani.” Sifa za mavazi kwa mujibu wa maandiko matakatifu ni KUJISITIRI (yafiche sehemu zote zinazotakiwa kufunikwa), ADABU NZURI (yawafanye watu wakuheshimu) na MOYO WA KIASI (yasiwe ya kukufuru na kukosa kiasi). Kwa hiyo inafaa mavazi yanayovaliwa hadhari yasiwe yanayobana sana, yanayoonyesha maungo ya mwili na nguo za ndani (transparent) na yasiwe ya gharama kubwa ukilinganisha na utoaji wako kwa Mungu. Kuvaa dhahabu na lulu wakati unatoa shilingi 500 kwa Mungu au kuwasaidia masikini, ni laana. 1 Timotheo 3:7 “Tena imempasa kushuhudiwa mema na watu walio nje; ili asianguke katika lawama na mtego wa Ibilisi.”
Lakini pia kama kwa kuvaa kwako unamkosesha mwingine utatoa hesabu siku ya mwisho. Labda kama ni umbile lako ambalo hata ukivaa kwa heshima bado mwingine kwa udhaifu wake anakutamani. Mt 18:7 “Ole ni wa ulimwengu kwa sababu ya mambo ya kukosesha! Maana hayana budi kuja mambo ya kukosesha; lakini ole wake mtu yule aliletaye jambo la kukosesha!”
8. Kujirahisisha na kupenda misaada ya bure
Mithali 23:27 “Kwa maana kahaba ni shimo refu; Na malaya ni rima jembamba.” Lk 4:6,7 “Ibilisi akamwambia, Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo. Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako.” Kuna wapendwa wanapenda kujirahisisha sana kwa watumishi wakidhani wote ni wazima kiroho. Hata kama ni wazima kiroho lakini bado ni wanadamu ambao wanaweza kujaribiwa. Watumishi ambao ndoa zao zina mgogoro ni rahisi sana kujaribiwa kwa vile mtu akioa au kuolewa anakuwa na dhiki katika mwili kuliko anayeishi peke yake. 1 Wakorintho 7:28 “Lakini, kama ukioa, huna hatia; wala mwanamwali akiolewa, hana hatia; lakini watu kama hao watakuwa na dhiki katika mwili nami nataka kuwazuilia hayo.” Jambo la hatari zaidi ni kuzoea kuomba mtu wa jinsi nyingine misaada ya kifedha. Unaweza kulazimika kuilipia kwa njia nyingine. Waimbaji binafsi wamekuwa rahisi kuanguka kwa kutafuta wafadhili wa album zao. Anaitwa kwenye hoteli fulani ili akapewe pesa matokeo yake anatoka na pesa akiwa amemuuza Yesu. Ukimuomba mtu akakusaidia, anakuwa na mamlaka juu yako. Ni vizuri zaidi kushirikisha watu wa Mungu na kumuomba Mungu na usikubali mtu yeyote ajione ni mfadhili wako. Yesu hajaishiwa kiasi hicho. Anaweza kuinua watu kwa ajili yako. Isaya 43:4 “Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na kabila za watu kwa ajili ya maisha yako.” Katika kila huduma Mungu ameandaa watu wenye nia njema wa kuitegemeza. Hakuna sababu ya kusumbuka kana kwamba unafanya biashara. Kama uimbaji wako ni biashara endelea ila hutakuta thawabu yoyote mbinguni maana umeshalipwa duniani. Wafilipi 4:6 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.” Mt 6:2-4 “Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu. Amin, nawaambieni, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume; sadaka yako iwe kwa siri; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.”
MADHARA YA UZINZI KWA MUHTASARI
1. Unaunganishwa na nafsi za watu wenye laana na matatizo mbalimbali (soul ties). 1 Wakorintho 6:16 “Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja.” Kama KIMWILI unaweza kuambukizwa UKIMWI au magonjwa ya ngono, katika NAFSI unaweza kuambukizwa laana za kutofanikiwa. Kuna mtu tangu azini (atoke nje ya ndoa yake), amekuwa akikojoa kitandani hadi alipoombewa.
2. Unakuwa mtumwa. Huwezi kutulia vizuri kwa vile unatafakari mambo ya zinaa muda wote. Matokeo yake huwezi kuwa na maendeleo yanayoendana na kipato chako. Huwezi kutosheka kwa vile umefungwa (addict). Tambua kwamba huwezi kupewa kitu na shetani bure. Lazima kuna siku utalipia. Waliomtumikia shetani kwa uaminifu katika eneo hili shetani hajawahi kuwathamini ndio maana amewapa UKIMWI, aibu, kipigo, utasa nk. Unakuwa mtumwa wa picha za ngono na kamwe huwezi kutosheka. Zaidi sana utatawaliwa na masturbation (punyeto) hadi utakapoathirika kimwili na kisaikolojia (maana kiroho umekufa kitambo).
3. Unakuwa na hatia. Kwa vile umesababisha ndoa ya mwenzako iwe mbaya na watoto wasisome unajisikia hatia. Kwa uliye na ndoa unajisikia hatia jinsi unavyoshindwa kusaidia familia yako na hujui utatokaje katika hali hiyo. Lakini pia kila mara unajisikia hatia moyoni kwamba ukifa leo utakwenda motoni. Hujiamini na unajiona kama uko uchi.
4. Unadharaulika na unaweza kukosa baraka zako. Sijaona watu wakimsifia kahaba na mzinzi hata kama wao wenyewe wako hivyo. Matokeo yake anaweza kutokea mtu sahihi wa kukuoa au kuolewa na wewe lakini avunjwe moyo na tabia zako au ushuhuda wako. Wazo lako zuri linawezwa kupuuzwa kwa vile una historia mbaya.
5. Unaweza kuibiwa mafanikio (nyota) yako na kujikuta kila unachofanya hakiendi kama mwanzo. Wakati huohuo mpenzi wako aliyekuibia kibali anaanza kufanikiwa sana wakati mwanzoni alikuwa hana mbele wala nyuma.
Mungu atusaidie na kutuvusha katika kipindi hiki ambacho shetani anafanya kazi kwa juhudi kubwa akijua ana muda mchache sana. Shetani ameachia mawakala wengi mpaka makanisani ili waimbe kwaya, waongoze sifa, wahudumie watumishi, wawe wafadhili ili mradi tu parapanda ikilia wengi wasiende na Bwana.
Najua sio wote mtapenda ujumbe huu lakini lazima niseme ukweli niliofunuliwa ili nisije nikadaiwa siku ya hukumu.
Lakini tukimuishia Bwana wetu Yesu Kristo tunakuwa ZAIDI YA WASHINDI. Warumi 8:37 “Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.”