Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 4:40 pm

KIGWANGALLA "MIMI SIHONGEKI, KWAHIVYO SIKO TAYARI KUNG'OKA KWA SABABU YOYOTE ILE"

Waziri Mpya wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangalla amesema kuwa ataendele kusalia katika wizara hiyo kama kilichowafanya watangulizi wake kuondoka ni masilahi yao binafsi, kwa kuwa yeye hahongeki, hashawishiki na aliyemteua analifahamu hilo.


“Mimi sihongeki, kwa hivyo siko tayari kung’oka kwa sababu yoyote ile, kama ni umasikini ni bora kufa njaa, kwangu fedha haiwezi kunitolea heshima licha ya kuwa wote tunazitaka,’’ amesema Dk Kigwangalla leo Jumapili Oktoba 22,2017 mjini Dodoma
Waziri huyo amejisifu kuwa hata aliyemteua anajua yeye ni muarobaini, hivyo imani yake ni kubwa kwake na kwa upande wake hatakuwa tayari kuona akiharibikiwa njiani.

Kigwangalla amesema kuwa yeye ni mtu ambaye hashawishiki na pesa kwahiyo yupo pale kufanya kazi tu “Sitakuwa tayari kupoteza heshima yangu, aliyeniteua anajua kuwa mimi ni muarobaini wa hayo yote, hata nilipoteuliwa walianza kunidhihaki kupitia mitandao ya kijamii kuwa ninakwenda kuharibikiwa huko, eti kwa sababu mawaziri hawadumu, haipo hiyo,” .

Mawaziri waliowahi kuiongoza wizara hiyo ni Anthony Diallo (2005-2006), Profesa Jumanne Maghembe (2007-2008; 2016-2017), Shamsa Mwangunga (2008-2010), Ezekiel Maige (2010-2012), Balozi Hamis Kagasheki (2012-2013) na Lazaro Nyalandu (2014-2015).
Meya Lazaro amesema baadhi ya mawaziri wamekuwa wakiitwa na makundi mbalimbali akitoa mfano wa wawindaji na kuzungumza nao lakini hushawishika kuegemea huko na wakiitwa na watu wengine huegemea huko, hivyo kushindwa kubaki katikati ya sekta zote.
Akijibu hoja hiyo, Dk Kigwangalla amesema hana shaka ya aina yoyote kuhusu kupewa wizara hiyo.
Dk Kigwangalla amewatahadharisha wadau akisema wanapofika ofisini kwake wajiandae vyema, vinginevyo anaweza kusimama na kumuacha mtu kama atagusa suala la rushwa.