Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 1:51 pm

DR MPANGO: MARUFUKU TRA KUFUNGA MADUKA YA WAFANYABIASHARA KUANZIA SASA

Dodoma: Wizara ya Fedha nchini Tanzania imeipiga marufuku Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufunga maduka na biashara za watu kwa kisingizio cha kutolipa kodi, na badala yake wametakiwa kukaa meza moja na wafanyabiashara ili kujadiliana nao namna ya kuilipa kodi ya serekali.

Agizo hilo limetolewa jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango wakati akitoa taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa na utekelezaji wa bajeti ya Serikali katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2018/19.

“Utaratibu wa kumfungia biashara mfanyabiashara anayedaiwa kodi ili kumshinikiza alipe sasa usitishwe mara moja, isipokuwa kwa wakwepa kodi sugu na hapo lazima kuwe na kibali cha kamishna wa mkuu wa TRA, nataka mjikite katika kutoa elimu siyo vitisho,” alisema Dk Mpango.

Aidha Waziri Mpango alikemea vikali matumizi mabaya ya lugha, vitisho na ubabe dhidi ya walipakodi wenye historia nzuri akitaka yasipewe nafasi na itakapothibitika mtumishi wa TRA amekwenda kinyume awajibishwe kwa kuzingatia tararibu za kiutumishi.

Dk Mpango alisema hata Rais John Magufuli amekwishaagiza utaratibu wa kufungia maduka usitishwe alipofungua kikao kazi cha TRA Desemba 10, hivyo amri hiyo inapaswa kutekelezwa.

Waziri huyo aliagiza TRA kujikita katika kutoa elimu kwa wafanyabiashara ili waone faida na thamani ya kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi yao na akawataka kupambana na wakwepa kodi hasa katika maeneo ya bandari bubu ambako alisema dawa yao ni kuwalipisha kodi na kutaifisha bidhaa zilizokwepa kulipiwa.