- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
AFYA: FAIDA ZA KULA MSOSI KIPORO.
Je wewe unapenda kiporo? Basi leo nina habari njema juu ya kiporo unachokula.
Tamaa kubwa ya watu wengi iko kwenye chakula. Wengi tunapenda kula vizuri kuliko kitu kingine chochote kile maishani. Ukiangalia uswahilini kwetu ugomvi mkubwa huanzia kwenye chakula, ndoa huanza kupata nyufa kutokana na chakula na mengine mengi tu yanaanzia kwenye chakula. Uswahilini kwetu chakula ndio hutawala maisha.
Mie nadhani hii inatokana na ukweli kuwa chakula ndio kitu pekee kinachoweza kumfanya mtu ajisikie vizuri katika ngazi yeyote ile ya maisha. Ukila vizuri unajisikia vizuri na afya tele, hata kama ni mara moja kwa mwaka. Lakini kuna tatizo kwenye kupenda sana kula, hasa vile vyakula visivyofaa kwa matumizi ya binadamu, utaishia kuongeza uzito ambao una madhara makubwa kwenye afya yako.
Lakini leo hatuzungumzii kula vizuri, wala kunenepa, bali tunaangalia njia ya kula chakula vizuri na kuwa na uhakika wa kutoongeza kalori (carolies) nyingi mwilini, hivyo kukufanya uwe na afya zaidi. Na mada yetu inahusu zaidi kwenye kula viporo - iwe wali maharage, tambi au vyakula vingine vingi.
ANGALIZO: Ukimaliza kusoma hii habari, kimbilia kiporo chako cha wali na maharage na ukile hadi ukinai, maana ni habari njema kwa wale wanaopenda kula bila kuongeza kilo kwenye miili yao. Kuwa makini tu jinsi ya kupasha moto.
Kula vyakula vilivyotoka kuandaliwa ni salama na afya zaidi, hii haina ulazima wa ufafanuzi. Lakini kuna jamii ya vyakula ambavyo ni vizuri zaidi kula vikiwa kama viporo. Aina mojawapo muhimu sana la hivi vyakula ni kundi la vyakula vya wanga (carbohydrates).
Tunakula vyakula vya wanga mara nyingi sana kwenye milo yetu ya kila siku. Ukila vyakula vya jamii ya wanga unaongeza kiwango cha sukari kwa kasi sana kwenye damu, wakati wa mmeng'enyo, hivyo hulazimu mwili kufanya kazi ya ziada ya kutoa kimeng'enyo cha insulin kinachofanya kazi ya kupunguza sukari kwenye damu. Hii kupanda na kushuka kwa damu kwa kasi husababisha chakula kusagwa haraka sana na unaweza kusikia njaa muda mfupi baada ya kula. Hii pia ni jibu mojawapo kwanini unasikia usingizi ukiwa umetoka kula chakula cha wanga - sukari na mwili kufanya kazi kwa nguvu - hukufanya kuwa na uchovu na uvivu.
Lakini, leo nna habari tofauti. Imefanyika utafiti na inaonyesha kuwa kuna utofauti wa umeng'enyaji kati ya wanga uliopikwa (wa mtoto), uliopoa na ule uliopoa na kupashwa moto. Hii ni kutokana na utafiti uliofanywa na kuripotiwa na BBC hapa. Utafiti unaonyesha kuwa kiwango cha mmeng'enyo na sukari kwenye damu kinapungua kama wanga ikipikwa na kuliwa kama kiporo (baridi), lakini hupunguza zaidi kiwango cha sukari kwa asililia 50% kama ikiwa kiporo na kupashwa moto. Hii ni kutokana na virutubisho vingi kutomeng'enyeka kirahisi baada ya wanga kupoa na kupashwa moto. Utafiti huu ulifanywa kwa kutumia tambi, lakini hii ni tabi aya vyakula vingi aina ya wanga.
Hii inamaanisha nini kwako wewe mlaji?
Utafiti huu unatoa ufafanuzi mzuri juu ya vyakula tunavyokula. Kutokana na matokeo haya, ni vizuri zaidi kula na kushiba kiporo cha jamii ya wanga sababu hakitokufanya uongezeke uzito kama utakapokula chakula cha kawaida. Hii ni kwa sababu nusu ya chakula unachokula ndio kinachotumika kukupa karoli mwilini na kilichobaki huishia kutoka kama makapi.
Watu wengi sana wanapenda kupunguza uzito bila kuvuruga kula, hii inawezekana kama utafanya mazoezi magumu na ya muda mrefu. Lakini kwa kupata matokeo mazuri zaidi, kupunguza kula vyakula visivyo na afya ni kitu muhimu zaidi kuliko hata mazoezi. Nasema hivi sababu chakula ndio kinachokufanya uongezeke uzito, lakini si swala la kujinyima kula, ni swala la kujua jinsi ya kula vyakula visivyokufanya unenepe. Vyakula vya kuzuia ni chumvi, sukari, na mafuta yasiyo na afya kama yalivyoelezewa hapa. Lakini leo unaongeza kiporo kwenye orodha ya vyakula vya kula bila kuwa na wasiwasi wa kunenepa.
Unaweza kuwa na swali, je kwanini ukila kiporo huwa nahisi kuvimbiwa na tumbo kujaa? Jibu ni rahisi, na sababu pekee ni kuwa unakosea kupasha moto kiporo chako, na jibu liko hapa chini. Lakini kwanza tuangalie jinsi ya kuhifadhi kiporo.
Je unahifadhi vipi kiporo ?
Ili kuzuia madhara ya kula chakula kisicho bora, kuwa makini kwenye kuhifadhi chakula vizuri. Ili kuhifadhi chakula chochote ni lazima kukiweka kwenye mazingira yanayozuia wadudu kuzaliana. Hivyo basi, ili kulinda chakula muda mrefu na kuepukana na madhara ya kuingiwa na vijidudu vinavyoweza kuleta sumu, weka chakula kwenye jokofu mara tu baada ya kumaliza kula. Vyakula vingi huharibika haraka na kuingiwa na wadudu mara tu vikishapoa, hasa vyakula vyenye protini ambavyo huharibika haraka sana vikihifadhiwa vibaya. Ni vizuri kulinda afya yako kwa kuhakikisha chakula kimehifadhiwa vizuri ili kuweza kuliwa wakati kinapohitajika.
Jinsi ya kupasha moto kiporo
Je unapasha moto vizuri kiporo chako?
Inawezekana ukaona ni swali lisilo na msingi, lakini mara nyingi wengi wetu hatufahamu jinsi ya kupasha moto kiporo. Wengi huweka jikoni na kuwa na papara ya kula kabla hakijapata moto vizuri. Hii si sawa, sababu kila chakula huwa na masharti yake kwenye kupasha moto. Moto husaidia kuamsha virutubisho na vilevile kuua vijidudu vilivyozaliana kwenye chakula.
Ukiwa unapasha moto kiporo cha wali, ni vizuri ukakiweka jikoni muda mrfu ili kipate moto vizuri. Hii ni muhimu sana, siyo tu kuua vijidudu, bali hukuwezesha kupata urahisi kwenye kukisaga chakula tumboni.
Chakula kikiwa hakijapata vizuri moto hukufanya kujisikia uvivu na hamu ya kulala. Ndio maana mara nyingi watu wengi huingiwa na uvivu na kupenda kulala baada ya kula kiporo kizito cha wali maharage asubuhi. Mie pia imeshanitokea mara nyingi na huwa napenda sana kiporo cha ubwabwa maharage, hasa yakiwa ya nazi.
Njia nzuri ya kuhakikisha unapasha moto chakula vizuri ni kuwa na microwave. Pasha moto kwa muda usiopungua dakika 4 ili kupata matokeo mazuri. Kama unatumia jiko la kawaida, ni vizuri ukaweka jikoni kwa muda na kuhakikisha chakula kinapata moto vizuri kabla ya kukitenga na kula.