- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
UTAFITI: SABABU NA MATIBABU YA TATIZO LA KUFIFIA KWA NURU YA MACHO
Lakini kufifia kwa nuru ya macho pia kwaweza kuwa dalili ya matatizo mengine ikiwa ni pamoja na magonjwa yanayohatarisha uoni wa macho na matatizo ya mishipa ya ubongo. Tatizo la kufifia kwa uoni laweza kuathiri macho yote mawili lakini baadhi ya watu hupata tatizo hili katika jicho moja tu.
Kuona mawingu-mawingu (mawimbi-mawimbi) ambapo vitu hufifia na kuona vitu vya ‘maziwa-maziwa’, mara nyingi, huchanganywa kimakosa na uoni hafifu wa macho.
Uonaji wa mawingu-mawingu (mawimbi-mawimbi) ni dalili ya matatizo fulani kama vile mtoto wa jicho (cataract). Uoni hafifu na uonaji wa mawingu-mawingu vyote, mara nyingi, huweza kuwa dalili ya tatizo kubwa la macho.
Daktari wa macho anaweza kupima kiwango cha kufifia kwa nuru ya macho yako na kubaini sababu kwa kukufanyia uchunguzi kamili ikiwa ni pamoja na vipimo vya spatial contrast sensitivity, slit-lamp na Standard Snellen. Kufifia ghafla kwa uoni wa macho kwaweza kuwa ni dalili ya tatizo jingine kubwa la kiafya, unapaswa kumuona daktari haraka.
Sababu na Matibabu ya Uoni hafifu wa Macho
· Myopia (uoni wa karibu)- Kufifia kwa nuru ya macho kwaweza kuwa dalili ya mayopia (macho kuweza kuona karibu tu), pamoja na makengeza, presha ya macho na maumivu ya kichwa. Myopia ndilo tatizo linalofahamika zaidi ambapo vitu vya mbali hufifia. Miwani, lensi na upasuaji kama vile LASIK na PRK ndizo njia zinazotumika sana kurekebisha tatizo la uoni wa karibu.
· Hyperopia (shida ya kuona vitu vya karibu) ni tatizo ambalo vitu vya mbali huonekana kwa macho makali kabisa lakini macho hayo hayo hushindwa kuona vitu vya karibu kabisa, au kuona huko vitu vya karibu husababisha hali isiyo ya kawaida ya msongo na uchovu wa macho. Tatizo hili linapocharuka, hata vitu vya mbali navyo hufifia. Mithili ya myopia, tatizo hioli nalo laweza kurekebishwa kwa miwani, lenzi, na upasuaji wa macho.
· Astigmatism- Hili ni tatizo la kufifia kwa macho katika masafa yote (karibu au mbali). Mara nyingi husababishwa na umbile lisilo la kawaida la konea (cornea).
Kutokana na tatizo hili, miale ya nuru (mwanga) hushindwa kuja katika kituo kimoja cha uoni kwenye retina ili kuleta uoni mzuri, hii haijali kitu kinachoonwa kiko umbali gani. Kama yalivyo matatizo ya kuona karibu na kuona mbali, tatizo hili la astigmatism nalo laweza kurekebishwa kwa miwani, lenzi au upasuaji wa macho.
· Presbyopia: ikiwa umefikisha umri wa miaka 40, na unaanza kupata tatizo la kupoteza nuru ya macho kwa vitu vya karibu-kama kushindwa kuona saizi ndogo za herufi za gazeti au maandishi mengine, basi hii ni dalili ya tatizo la presbyopia, ambalo, kimaumbile, ni tatizo linalojitokeza kwa sababu ya umri.
Wakati ambapo dalili za tatizo hili la presbyopia ni sawa tu na zile za hyperopia (kufifia kwa uoni wa karibu, msongo wa macho wakati wa kusoma), tatizo hili la presbyaopia ni kupungua kwa uwezo wa kuona vitu vya karibu kutokana na kuwamba kwa lenzi ndani ya macho badala ya hitilafu ya uoni inayosababishwa na umbile la jumla la jicho kama hyperopia.
Tatizo la presbyopia humuathiri karibu kila mtu anayevuka miaka 45. Watu wengi hutumia miwani ya kusomea. au lenzi zenye kukuza herufi (bifocal au progressive lenses).
Lakini pia kuna tiba za upasuaji macho kwa tatizo hili kama vile movision LASIK na Conductive keratoplasty. Hii ni kwa watu ambao tiba hiyo inawafaa.
· Tatizo sugu la Ukavu wa Macho- tatizo hili (chronic dry eye) huyaathiri macho yako kwa namna nyingi ikiwa ni pamoja na kufifiliza na kubadilisha-badilisha uoni wa macho. Wakati ambapo machozi ya bandia (artificial tears) huweza kusaidia, tatizo la ukavu wa macho linapozidi kiwango laweza kuhitaji dawa za kuandikiwa na daktari au vilainishio vya kulainisha macho na kuyaweka katika afya nzuri. (punctal plugs).
· Ujauzito. Kufifia kwa uoni wa macho ni tatizo la kawaida katika kipindi cha ujauzito na wakati mwingine huambatana na uoni wa vitu viwili-viwili-kuona dabodabo (diplopia). Mabadiliko ya homoni huweza kubadili muundo na upande wa konea ya jicho lako, na kusababisha uoni wako kufifia. Ukavu wa macho pia ni jambo la kawaida kwa akina mama wajawazito na huweza kusababisha uoni hafifu wa macho.
· Mara zote unapaswa kuripoti kwa daktari matatizo yoyote ya macho katika kipindi cha ujauzito. Wakati ambapo uhafifu wa kuona, katika baadhi ya kadhia, si jambo la kutisha, lakini kwaweza kuwa dalili ya magonjwa ya kisukari na shinikizo la juu la damu.
· Maumivu makali ya macho (Ocular migraines) yanayomfanya mtu asikie homa au ashindwe kuona vizuri: Kufifia kwa nuru ya macho, kuchomwa moja kwa moja na mwanga wa jua, kuona zigizaga zote huwa ni dalili za kawaida kabla ya kuanza kwa maumivu ya macho.
· Kuelea-elea kwa tishu jichoni (Eye floaters). Uoni wa macho yako waweza kufifilizwa na vicheche-cheche vidogovidogo vya muda (floaters) katika eneo la uoni wa macho. Kwa kawaida vicheche-cheche hivyo hujitokeza pale kioo cha macho kinapoanza kufifia kwa umri na kusababisha chembechembe za tishu ndani ya kioo cha jicho kuelea-elea ndani ya jicho na kusababisha vivuli kwenye retina. Kama una umri wa kawaida, na unaona dalili za tatizo hili, muone daktari haraka.
· Kufifia kwa Macho baada ya Upasuaji (LASIK): Uoni wako wa macho unaweza kufifia muda mfupi baada ya upasuaji wa LASIK au aina nyingine za upasuaji wa macho. Yapasa uoni wa macho uwe tena mzuri ndani ya siku mbili baada ya upasuaji, lakini yaweza kuchukua majuma kadhaa uoni huo kutengemaa barabara.
· Matone ya Macho na Dawa: baadhi ya matone ya macho hasahasa dawa zinazowekwa kemikali za kuhifadhia zisiharibike (preservatives) huweza kusababisha macho kuwasha na nuru yake kufifia. Kwa kiasi kikubwa, madhara haya yanaweza kudhibitiwa kwa machozi ya bandia, dawa za ukavu wa macho au vilainishi (punctal plugs).
· Pia baadhi ya dawa kama vidonge vya mzio (allergy pills) huweza kusababisha madhara ya ukavu wa macho na kufifia kwa nuru ya macho. Katika kipindi cha uchunguzi kamili wa macho, daktari wako wa macho anaweza kukushauri iwapo dawa zinaweza kusababisha uoni wako wa macho kufifia.
· Kuvaa-vaa sana lenzi za macho: Kuvaa sana lenzi za macho (miwani ya kukuzia maandishi) zaidi ya vile alivyokushauri daktari wako kwaweza kusababisha madhara katika lenzi zako za macho. Madhara hayo ni pamoja na kufifia kwa nuru ya macho na maambukizi ya macho.
Dalili za tatizo kubwa la Macho
· Matatizo na Magonjwa ya macho: Unapoondokewa kwa ghafla na nuru ya kuona katika jicho moja pale unapokuwa na zaidi ya miaka 60, huenda umepata tundu katika sehemu ya retina ambako ndiko uoni mzuri wa macho unakotokea. Kufifia kwa nuru ya macho pia kwaweza kuwa dalili ya kioo cha jicho (retina) kubanduka, malengelenge ya macho (eye herpes) au tatizo la mshipa wa macho (optic nerve) pamoja na sababu nyinginezo.
Baadhi ya matatizo na magonjwa ya macho huweza kusababisha kupotea moja kwa moja kwa uoni wa macho, hivyo ni muhimu kuwa karibu na daktari wako kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.
Mtoto wa jicho (Cataracts): Mabadiliko ya nuru ya macho kama vile kufifia au kuona mawingu-mawingu yaweza kuwa dalili ya mtoto wa jicho. Matoto ya macho yasipoondolewa, hatimaye hutanda kama wingu na kuziba uoni wa macho kwa kiwango cha upofu. Lakini kwa kuweka lenzi za bandia mahali pa matoto ya macho, upasuaji huwa unafanikiwa sana kurejesha uoni uliopotea wa macho.
· Glaucoma: Kufifia kwa nuru ya macho kwaweza kuwa dalili ya glaucoma. Dalili hizo zaweza kujumuisha kunywea kidogokidogo au kwa ghafla kwa eneo la kuonea ndani ya jicho kukiambatana na uonaji hafifu katika kingo za chumba chako cha kuonea. Bila kupata tiba, hali ya kupoteza nuru ya macho itazidi kuendelea na matokeo yake ni upofu wa maisha.
· Udhaifu wa Macho utokanao na Umri: Kupoteza nuru ya macho ikiwa ni pamoja na kuona mistari iliyonyooka imepinda-pinda au imekatika-katika, kwaweza kuwa ni dalili ya udhaifu utokanao na umri, na ndiyo sababu kuu ya kupofuka macho kwa wazee wenye umri mkubwa.
· Kisukari cha kuhatarisha macho (Diabetic retinopathy): Kama una kisukari, kufifia kusikoeleweka kwa uoni wa macho kwaweza kuwa ni dalili ya ugonjwa huo kuharibu kioo cha jicho (retina)
· Magonjwa ya Moyo na Magonjwa mengine ya Kimfumo: Kufifia kwa macho kunakoambatana na kuona vitu viwili-viwili, kwaweza kuwa ni dalili ya tatizo la ghafla la kiafya kama vile kiharusi au kuvuja kwa damu ubongoni. Ukiona una tatizo hilo, wahi haraka kuonana na daktari.
· Unapokuwa na uoni hafifu unaokuja na kuondoka, basi hiyo ni dalili ya uchovu tu wa mwili na kukaa sana juani au msongo wa macho. Hata hivyo ufifiaji wa ghafla au endelevu wa nuru ya macho pia waweza kuwa dalili ya ugonjwa mkubwa wa macho au tatizo jingine la kiafya. Yanapokea mabadiliko ya ghafla ya uoni wa macho, wahi kumuona daktari.