Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 1:18 am

UTAFITI: FAIDA NA HASARA ZA KULA UBUYU KIAFYA.

Ubuyu ni tunda ambalo hupatikana katika miti jamii ya adansonia. Ubuyu umekua na matumizi mbalimbali wengi tukiutumia kama matunda. Wengine hutumia juisi yake kutengenezea barafu (ice cream). Pia ili kuongeza ladha wengine huchanganya ubuyu na viungo mbalimbali ili kuongeza ladha ya ubuyu.


Kabla ya kuangalia nini faida na hasara za kula ubuyu kwanza tuangalie ubuyu una viirutubisho gani.


Katika tunda hili la ubuyu kuna :-


  • 1.Protini.
  • 2.Wanga.
  • 3.Vitamini B2.
  • 4.Vitamini C.
  • 5.Madini ya kalshamu.
  • 6.Madini ya magnesiamu.
  • 7.Madini ya potasiamu.
  • 8.Madini ya chuma.
  • Hivyo ni baadhi ya virutubisho ambavyo hupatikana kwa wingi katika ubuyu.

    Kulingana na virutubisho hivyo vinavyopatikana katika ubuyu tuangalie faida na hasara zake katika mwili wa binadamu.


    FAIDA ZA KULA UBUYU.

    Kikubwa hasa ubuyu katika mwili una uwezo mkubwa wa kuimarisha kinga ya mwili, kuimarisha mifupa, kusaidia mfumo wa umeng’enyaji tumboni, kupunguza maumivu na uvimbe na kusisimua utengenezaji wa seli na tishu mpya . Pia kusaidia kupunguza shinikizo la damu na kuzuia magonjwa sugu.


    Ubuyu una kiwango kikubwa sana cha madini ya potasiamu. Kutokana na uwepo wa madini haya kunapelekea ubuyu kuwa na faida kubwa katika afya ya moyo kwasababu huusaidia moyo kwa kiasi kikubwa kusukuma damu.


    Pia madini haya ya potasiamu husaidia kutanua mishipa ya damu hivyo kuifanya damu kupita kirahisi katika mishipa ya damu, kwa hali hiyo hupunguza hatari ya mtu kupata shinikizo la damu (BP).


    Pia kuna madini haya ya kalshiamu na magnesiamu ambayo hupatikana kwa wingi katika ubuyu. Madini haya huusika kwa kiwango kikubwa katika uimarishaji wa mifupa. Madini haya ni muhimu hasa kwa wazee na watoto kwa kuwa mifupa yao kulingana na umri wao inahitaji madini haya kuimarika. Kwa watoto mifupa yao inahitaji madini haya kuweza kukua vizuri na kuzuia matatizo ya matege.


    Kutokana na ubuyu kuwa na kiwango kikubwa cha madini ya chuma hupunguza hatari ya kupata magonjwa ya upungufu wa damu (Anemia). Kwasababu madini ya chuma huusika katika uzalishaji wa seli nyekundu za damu. Pia kwa mgonjwa wa upungufu wa damu mwilini kwa kutumia ubuyu kutamsaidia kuweza kurejesha kiwango chake cha damu mwilini.


    Mbali na madini hayo pia ubuyu una nyuzi lishe (fibers). Nyuzi lishe hizi husaidia hasa katika mfumo wa mmeng’enyo wa chakula. Huondoa maumivu wakati wa haja (constipation). Nyuzi lishe hizi pia ni msaada mkubwa katika kurekebisha kiwango cha sukari mwilini, kiwango cha lehemu (cholesterol) vilevile nazo husaidia katika kuboresha afya ya moyo.


    Mbali na nyuzi lishe ubuyu una viondoa sumu (anti – oxidants). Viondoa sumu hivi husaidia kuondoa sumu mbalimbali katika mwili hivyo husaidia kuukinga mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali pia kuukinga mwili dhidi ya saratani (cancer).


    Vitamin C hupatikana pia katika ubuyu. Vitamini C husaidia mwili kuzalisha seli nyeupe za damu kwa wingi. Seli hizi nyeupe za damu huusaidia mwili kuimarisha kinga yake dhidi ya magonjwa mbalimbali.


    Mbali na kuimarisha kinga ya mwili vitamini C husaidia katika uzalishaji wa Collagen. Uzalishaji wa Collagen mwilini huusaidia mwili kuongeza ufanisi kwa utendaji kazi wa mifumo mbalimbali ndani ya mwili. Pia husaidia kupona kwa majeraha kwa haraka.


    Hizo ni baadhi ya faida ambazo unaweza kuzipata kiafya kwa kula ubuyu.

    Mpaka sasa hakuna matatizo yoyote yaliyobainika kwa mtu kula ubuyu isipokuwa mafuta kutokana na mbegu za ubuyu yamebainika kuwa na kemikali ijuikanayo kwa jina la Cyclopropenoid fatty acids (CPFA).


    Kemikali hiyo katika tafiti mbalimbali imegundulika kusababisha ugonjwa wa ini pamoja na saratani(cancer).