Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 11:29 am

UTAFITI: DALILI ZA MAGONJWA YA ZINAA

Kuna magonjwa mengi tofauti ya zinaa, lakini yale ambayo yameenea sana ni kisonono, kaswende, klamdia, kankroidi, utando mweupe , Virusi vya UKIMWI na UKIMWI. Shida kubwa ya magonjwa mengi ya zinaa ni kwamba dalili zake hazionekani kwa urahisi na kama yasipotibiwa kikamilifu yanaweza kuleta madhara makubwa. Maelezo kuhusu magonjwa ya zinaa yaliyoenea sana ni kama yafuatayo:

Kisonono:

Huchukua muda wa siku 1 hadi 14 tangu kuambukizwa mpaka kuonyesha dalili za kuumwa. Kwa wanawake dalili za kisonono ni maumivu chini ya tumbo ambayo yanaweza kuambatana na homa na kutokwa uchafu ukeni. Wapo wanawake wengine ambao hawaoni dalili zozote. Kwa wanaume dalili ni kutokwa na usaha uumeni na kupata maumivu wakati wa kukojoa. Athari yake kwa mwanamke ni kuziba mirija ya kupitisha mayai na mimba kutunga nje ya mfuko wa uzazi, na vilevile ugumba. Kwa mtoto aliye tumboni mwa mama mjamzito kisonono cha mama yake kinaweza kusababisha upofu. Kwa mwanaume athari yake ni kuziba mirija ya kupitisha mkojo.

Kaswende:

Dalili ya kaswende kwa mwanamke ni vidonda sehemu za siri hasa kwenye mashavu ya uke na sehemu ya njia ya haja kubwa, pamoja na sundosundo sehemu ya siri. Kwa mwanaume dalili ni vidonda. Mara nyingi kimoja kwenye kichwa cha uume, kwenye kishina cha uume na kuzunguka njia ya haja kubwa. Pia mwanaume anaweza kupata sundosundo sehemu za siri. Ugonjwa huu husababisha matatizo ya moyo, na kuharibu ubongo na kuzaa watoto walemavu.

Klamdia:

Dalili yake kwa mwanamke mara nyingi siyo rahisi kuonekana. Kwa mwanaume dalili ni kupata maumivu wakati wa kukojoa, na kukojoa mara kwa mara. Athari kwa mwanamke ni kuziba kwa mirija ya kupitisha mayai na mimba kutunga nje ya mfuko wa uzazi. Mimba hizi kuhatarisha maisha ya mama na kuleta ugumba vinaweza kutokea. Kwa mwanaume athari ni kuziba mirija ya kupitisha mbegu na utasa.

Kankroidi:

Dalili yake ni vidonda sehemu za siri vinavyokuwa na maumivu makali, maumivu wakati mkojo unapopita kwenye vidonda na kuvimba tezi sehemu za siri. Tezi huweza kupasuka na kutoa uchafu na maumivu makali.

Utando mweupe:

Dalili kwa mwanamke ni kutokwa na uchafu ukeni (kama maziwa yaliyoganda), kuwashwa na kuwa na michubuko sehemu za siri. Kwa mwanaume ni kuwashwa sehemu za siri na kusikia maumivu wakati wa kukojoa. Athari ni maumivu wakati wa kujamiiana.

Virusi vya UKIMWI:

Katika hatua ya mwanzo baada ya kuambukizwa hakuna dalili maalum. Hatua hii inaweza kuchukua mpaka miaka kumi. Lakini mara mtu anapoanza kuugua UKIMWI dalili zinakuwa nyingi. Pamoja na kupungua kinga ya mwili, kupungua uzito na kuumwa mara kwa mara. Matokeo ya kuugua UKIMWI baada ya muda fulani ni kifo.