Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 9:47 am

TUNDU LISSU: WANATAKA KUNIFUTA UBUNGE KWA MABAVU, ITASHINDIKANA VILE VILE

Mbunge wa jimbo la Singida Mashariki kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amesema kuna mpango mkubwa wa siri wa kutaka kumvua ubunge wake, huku akikishutumu chama Tawala cha CCM kuwa ndio kinara wa kusuka mpango huo kwa kushirikiana na Serekali iliyopo madarakani kwasasa hapa nchini.

“NIMEPATA taarifa, kutoka kwa watu wawili tofauti, kwamba kuna mkakati unaandaliwa wa kunivua ubunge wa Jimbo la Singida Mashariki. Mkakati huo unaihusisha Ikulu ya Rais John Magufuli na uongozi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Spika Job Ndugai'' amesema Lissu

"Walitaka nife kwa risasi. Imeshindikana. Wakataka nife kwa kukosa matibabu na huduma nyingine kama mgonjwa. Ikashindikana. Sasa wanataka kunifuta ubunge kwa mabavu. Itashindikana vile vile" amesema Lissu

Lissu ambaye alikuwa Rais wa chama cha Wanasheria Tanzania (TLS) kwa sasa yupo kwenye matibabu nchini Ubelgiji anakopatiwa matibabu kufuatia kushambuliwa kwa risasi na wanaoitwa na serikali, “watu wasiojulikana,” miaka miwili iliyopita.

Lissu anasema hoja inayojengwa na wakubwa hawa ni kwamba yeye ni mtoro wa Bunge. Yaani hajamwandikia Katibu wa Bunge taarifa yoyote ya maandishi kuhusu kuumwa kwangu wala matibabu yangu. Kwa maneno mengine, hajahudhuria vikao vya Bunge tangu tarehe 7 Septemba 2017, hadi sasa bila sababu au taarifa yoyote rasmi.

Sina sababu yoyote ya kutilia shaka taarifa hizi. Walionipatia ni watu wenye dhamana kubwa bungeni na kwenye serikali ya Magufuli.

Sijashangazwa na kuwepo kwa mkakati huu. Visasi na chuki ndiyo umekuwa utamaduni wa kawaida ya serikali ya sasa inayoongozwa na John Pombe Magufuli. Kilichonishangaza ni hoja zinazojengwa kuhalalisha uovu huu."

Ni taarifa gani ya maandishi watu hawa wanahitaji wakati nilishambuliwa nikiwa kwenye vikao vya Bunge mjini Dodoma?

Nilipelekwa jijini Nairobi nchini Kenya, nikiwa sijitambui kutokea hospitali kuu ya mkoa wa Dodoma, baada ya kikao kilichomshirikisha Katibu wa Bunge wa wakati huo, Dk. Thomas Kashilila, Spika Ndugai na Naibu Spika Tulia Ackson.

Alikuwapo pia waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Dk. Ulisubisya Mpoki. Wengine waliokuwapo ni waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wakati huo, Dk. Mwigulu Nchemba; na nilisindikizwa mpaka Nairobi Hospital na daktari kutoka hospitali kuu ya mkoa wa Dodoma.

Wakati wote ambao nimekuwa kwenye matibabu uongozi wa Bunge umewasiliana kwa maandishi na mwakilishi wa familia yangu kuhusu matibabu yangu. Wametoa matamko mengi hadharani kuhusu kushambuliwa kwangu na kuhusu matibabu yangu.

Makamu wa Rais, Mama Samia Suluh Hassan, amekuja kuniona nikiwa hospitalini Nairobi; Balozi wa Tanzania Ubelgiji, Joseph Sokoine, amekuja kuniona hospitalini Leuven mara mbili.

Ni Spika Ndugai na uongozi wote wa Bunge, akiwemo Katibu wa Bunge, Steven Kagaigai, na maafisa wakae, ndio hawajawahi kukanyaga hospitalini kuja kumwangalia mgonjwa wao, aliyeumizwa vibaya akiwa bungeni.

Katika mojawapo ya barua alizowahi kuiandikia familia yangu, Katibu wa Bunge Kagaigai aliahidi kwamba timu ya madaktari bingwa kutoka hospitali ya Taifa ya Muhimbili ingekuja kunitembelea Nairobi au Leuven. Mwaka mzima umepita na sijawaona.

Ni wazi, kwa hiyo, kwamba uongozi wa Bunge haujawahi kujihangaisha na mimi na matibabu yangu kwa namna yoyote ile, zaidi ya kuninyima haki zangu za matibabu kinyume na Sheria ya Uendeshaji wa Bunge.

Katika mazingira haya, ni kitu gani ambacho hawakifahamu kuhusu kushambuliwa na kuumizwa kwangu, na kuhusu matibabu yangu, ambako kunahitaji waandikiwe barua rasmi?

Na waandikiwe barua gani zaidi ya barua nne au tano ambazo wamekwishaandikiwa na kaka yangu, wakili Alute Mughwai na ambazo wameshazijibu?

Ninachoona ni hiki: Walitaka nife kwa risasi. Imeshindikana. Wakataka nife kwa kukosa matibabu na huduma nyingine kama mgonjwa. Ikashindikana. Sasa wanataka kunifuta ubunge kwa mabavu. Itashindikana vile vile.

Badala ya kuona aibu na kukaa kimya, wanataka kuzima moto kwa kuumwagia petroli. Hautazimika, utawaka zaidi. Na, kwa kufanya hivyo, watajianika hadharani ili dunia nzima ishuhudie uovu wao!”