Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 5:02 am

TAKUKURU YAMSHIKILIA BABA NA MWANAE KWA KUMPA RUSHWA DC KATAMBI

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (Takukuru) Mkoa wa Dodoma inawashikilia watu saba kwa makosa mbalimbali ya rushwa ikiwemo Baba na mwanaye kwa kumhonga Mkuu wa Wilaya Patrobas Katambi kiasi cha Sh.Milioni 1.2 ili asiweze kutekeleza majukumu yake.

Akizungumza leo na waandishi wa habari, Mkuu wa Taasisi hiyo mkoani Dodoma, Sosthenes Kibwengo amesema katika tukio la kumhonga Mkuu wa wilaya taasisi hiyo imewapeleka mahakamani Mfanyabiashara Bahadur Abdallah Hijri(68) pamoja na mwanaye Nahid Bahadur Hijri(33) ambaye ni Mhasibu wa Kampuni ya Victory Bookshop Ltd ya jijini hapa.

Image result for DC Patrobas Katambi

Amesema watuhumiwa hao walinaswa Julai 27, mwaka huu majira ya saa 11 jioni katika Hoteli ya Royal Village.

Amedai kuwa watuhumiwa hao waliahidi na kutoa hongo ya kiasi hicho cha fedha kwa Mkuu wa wilaya ili asifuatilie mapungufu katika utekelezaji wa amri ya Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya juu ya kukazia hukumu iliyowasilishwa kwa Mfanyabiashara huyo na dada yake.

Image result for TAKUKURU DODOMA


“Baada ya kupata taarifa ya watuhumiwa kuahidi kutoa fedha hiyo kama kishawishi kwa Mkuu wa wilaya tulianza kufuatilia na kufanikiwa kuwakamata mara baada ya mtuhumiwa Nahid kumkabidhi Mkuu huyo rushwa hiyo,”amesema.

Amesema watuhumiwa hao wametenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 15(1)(a) na (b) vya sheria ya kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.